Doh! Diamond Platnumz ashtushwa na uzito wake mpya wa mwili

Diamond ameonekana kushangazwa sana na uzito mwingi ulioongezeka kwenye mwili wake.

Muhtasari

•Diamond alionyesha wazi kuwa uzito wake mpya ulimshangaza kwani hakutarajia kuwa mwili wake ulikuwa umefikia hapo.

•Siku ya Alhamisi asubuhi, bosi huyo wa Wasafi alifichua kwamba sasa ana uzito wa mwili wa takriban kilo sabini na nne.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Staa wa Bongo Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz anaonekana kushangazwa sana na uzito mwingi ulioongezeka kwenye mwili wake.

Siku ya Alhamisi asubuhi, bosi huyo wa Wasafi alifichua kwamba sasa ana uzito wa mwili wa takriban kilo sabini na nne.

Diamond alionyesha wazi kuwa uzito wake mpya ulimshangaza kwani hakutarajia kuwa mwili wake ulikuwa umefikia hapo.

"Doh! 73.9kg," aliandika chini ya video inayomuonyesha akiwa amesimama juu ya kifaa cha kupima uzito wa mwili na kuambatanisha ujumbe huo wake na emoji zinazoashiria mshangao mkubwa.

Haya yanajiri katika kipindi ambapo kumekuwa na wasiwasi mwingi kuhusu ukubwa wa mwili wa staa huyo wa Bongo. Katika siku za hivi majuzi, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitilia shaka hali ya afya ya mwimbaji huyo huku wakidai kuwa anaonekana mwembamba zaidi kuliko kawaida.

"Kuna siku tutakusanyika kujadili afya ya huyu mwamba, nipo palee," mtumizi mmoja wa Instagram aliandika chini ya chapisho la Diamond la hivi majuzi kwenye mtandao huo.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Maoni mengine mengi kama hayo yameonekana katika machapisho yake mengine kwenye kurasa zake mbalimbali za mitandao ya kijamii.

Hivi majuzi, bosi huyo wa WCB alidokeza kwamba mzozo wake wa muda mrefu na mwimbaji mwenzake Alikiba umefika kikomo.

Staa huyo alidokeza kwamba hali sasa ni shwari kabisa kati yake na Alikiba huku akimuonyesha upendo mkubwa kwenye Instagram.

Siku ya Jumapili, Diamond alikiri mapenzi yake makubwa kwa wimbo 'Asali' ambao mwenzake huyo aliutoa mwezi Septemba mwaka jana. Aliweka wazi kwamba hicho ndicho kibao cha Alikiba anachokipenda zaidi.

"Favourite 🏆🤍" (Wimbo pendwa) Diamond aliandika chini ya picha ya bango la wimbo huo wa Alikiba. 

Wengi wamechukulia hatua hiyo kama ishara kuwa Diamond hana kinyongo dhidi ya mwimbaji huyo mwenzake.

Wanamuziki hao wawili wakongwe wa Bongo wamekuwa wakidaiwa kuzozana kwa muda mrefu na mara kadhaa wamekuwa wakionyesha wazi ugomvi wao. Hata hivyo, wamezungumzia tofauti zao mara nadra tu

Katika wimbo wake wa ‘Nawaza’ alioutoa mapema mwaka jana, Diamond alikiri kuwa baada ya kuwaza kwa kina aligundua kwamba yeye na Alikiba wanatofautiana katika mambo madogo madogo kama mashabiki na umaarufu.

“Nilowaza leo nishawaza sana, mimi na Kiba ugomvi nikagundua ni ushamba na ujana wa kugombania mashabiki,” aliimba

Bosi huyo wa WCB alibainisha zaidi kuwa amekua katika tasnia ya muziki na hajishughulishi tena na masuala kama hayo.