Jackie Matubia: Nilianza mapenzi na Blessing Lungaho nikiwa na mpenzi mwingine

“Lakini hukusema hilo, uliniambia uko singo… kwa hiyo ulikuwa unaniingiza boksi, ni kama mimi ndio nilitongozwa…” - Blessing Lung’aho.

Muhtasari

• "Sikuwa nimetoka katika uhusiano huo wa kwanza hata kama hatukuwa tunaongea sana,” Jackie Matubia alitetea jibu lake.

Jackie Matubia asema alikuwa kwenye mapenzi alipompenda Lung'aho.
Jackie Matubia asema alikuwa kwenye mapenzi alipompenda Lung'aho.
Image: Instagram

Mwigizaji Jackie Matubia amepasua mbarika kwamba kipindi wanajuana na mpenzi wake wa sasa, Mwigizaji mwenza Blessing Lung’aho, tayari alikuwa katika uhusiano mwingine ambao alikuwa anauchorea hesabu ya kuuvunja.

Kupitia ukurasa wake wa YouTube, Matubia walikuwa wanashiriki kipindi cha maswali na majibu pamoja na mumewe, na Terrece Creative na mkewe Milly Chebby.

Familia hizo mbili zilikuwa zinaulizana maswali ya kifamilia kupitia kadi, na ulipofika wakati wa Chebby kulisoma swali lake, lilikuwa “umewahi chumbiana na mtu mwingine wakati bado uko katika uhusiano na mtu wa kwanza?”

Matubia alifunguka ukweli wake kwamba alipoanza kuchumbiana na Blessing, kipindi hicho alikuwa katika uhusiano na mtu mwingine.

“Ndio mimi nimewahi, wakati nilianza kuchumbiana na Blessing, nilikuwa katika uhusiano mwingine. Sikuwa nimetoka katika uhusiano huo wa kwanza hata kama hatukuwa tunaongea sana,” Jackie Matubia alisema.

Hata hivyo, Blessing alikanusha vikali akisema kwamba wakati alikuwa anajaribu kumtongoza, Matubia alimwambia alikuwa bila mpenzi, lakini wenzake wakamwambia kwamba ilikuwa njia moja ya kumuingiza kwenye boksi.

“Lakini hukusema hilo, uliniambia uko singo… kwa hiyo ulikuwa unaniingiza boksi, ni kama mimi ndio nilitongozwa…” Blessing Lung’aho alisema.

Blessing alijitetea kwamba alivutiwa kwa mkewe Matubia kwa sababu ya makalio, akisema kwamba yeye muda wote huvutiwa na makalio katika mwili wa mwanamke.

Wapenzi hao wawili walianza uhusiano wao wa mapenzi kipindi wakiwa wanaigiza katika kipindi cha Zora ambacho kilikuwa kinapeperushwa kila siku jioni katika runinga ya Citizen.

Kipindi hicho kilipofikia tamati yake, wapenzi hao walioana na mpaka sasa wana mtoto mmoja, hata hivyo Matubia alikuwa na mtoto mwingine kabla ya kukutana na kupendana na Blessing Lung’aho.