Sonko apoteza ukurasa wa Facebook wenye wafuasi 2.5M kwa kushambulia LGBTQ

Sonko alisema kwamba Facebook wanamtaka kuomba radhi na kutuma rufaa ili kurudishiwa ukurasa wake, jambo alilosema hawezi.

Muhtasari

• "Wamelalamika kwa Facebook mpaka ukurasa wangu wa wafuasi 2,500,000 umelemazwa na kufungwa" Sonko alilia.

Image: FACEBOOK// MIKE SONKO

Mfanyibiashara Mike Sonko amepata pigo baada ya mamlaka ya Meta, ambayo inamiliki mitandao ya Facebook, Instagram na WhatsApp kumfungia ukurasa wake wa Facebook.

Mfanyibiashara huyo aliyegeuka mwanasiasa alilalama kupitia ukurasa wake wa Twitter akisema kwamba Facebook walifunga ukurasa wake uliokuwa na wafuasi Zaidi ya milioni 2.5 kwa kile alisema kwamba ni kutokana na mwendelezo wa mashambulizi yake dhidi ya jumuiya la LGBTQ.

Gavana huyo wa zamani wa Nairobi alisema kwamba mamlaka hiyo ilimtaka kutuma msamaha kwao kwa kuendeleza kile walichotaja kama ‘chuki’ dhidi ya LGBTQ, jambo ambalo alisema hawezi fanya na kusema badala yake ataendeleza ajenda hiyo ya kuikashifu jamii ya LGBTQ kupitia ukurasa wa Twitter – Washidnani wa Meta.

“Hawa masonga wa LGBTQ wako na nguvu. Wamelalamika kwa Facebook mpaka ukurasa wangu wa wafuasi 2,500,000 umelemazwa na kufungwa eti hadi pale nitakapooomba radhi kisha nikate rufaa. Siwezi na sitawaomba msamaha. Hapa Tweeter mko wafuasi 2,300,000  na bado kukua kama moto wa kichakani. ALLUTA CONTINUA,” Sonko alisema.

Kwa muda mrefu, Mike Sonko amekuwa akipakia picha na video za wapenzi wa jinsia moja katika sehemu mbali mbali akionesha hadharani kutofurahishwa kwake na vitendo hivyo huku akiwabandika majina mbalimbali mabaya.

Nchini Kenya kwa takribani wiki tatu sasa, gumzo kuhusu suala zima la LGBTQ limekuwa tete kote mitandaoni haswa kufuatia uamuzi wa mahakama ya upeo kuhalalisha mikusanyiko ya LGBTQ nchini.