Amber Ray anaigiza maisha kuwafurahisha wanamitandao? EX wake ana fikira hizi

Amber Ray alikuwa gumzo la mitandaoni baada ya kulipia bango la barabarani kutangaza dhihirisho ya jinsia ya mtoto wake ajaye.

Muhtasari

• Kabba walichumbiana na Ray kwa muda mfupi zaidi mwaka jana kabla ya kuachana na kila mmoja kwenda na hamsini zake.

Aliyekuwa mpenzi wa Amber Ray anahisi anaigiza maisha.
Aliyekuwa mpenzi wa Amber Ray anahisi anaigiza maisha.
Image: Instagram,

Mpenzi wa zamani wa mwanasosholaiti Amber Ray, IB Kabba anaonekana bado kutoamini kwamba Ray alishamuacha na kusonga mbele na maisha yake akiwa na mpenzi mpya, Kennedy Rapudo.

Tangu mwishoni wiki jana Ray na Rapudo walipoteka anga za mitandao ya kijamii kwa kufanya bonge la tafrija ya dhihirisho ya jinsia ya mtoto wao, watu mbali mbali wamekuwa wakizungumza kwa maoni mseto.

Ray alifika kwenye tafrija hiyo kwa kutumia helikopta. Pia alitumia pesa nyingi kulipia bango la barabarani kutangaza dhihirisho la jinsia ya mwanawe.

IB Kabba, raia wa Sierra Leone ambaye ni mchezaji wa mpira wa vikapu, na ambaye wengi mlimjua kupitia uhusiano wake wa mapenzi na Amber Ray amekuwa mtu mwenye mawazo mengi ya chuki dhidi ya kitendo hicho.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kabba amekuwa akipakia video na machapisho ya maandishi ambayo yanakisiwa kumlenga Ray, japo hajakuwa akimtaja moja kwa moja.

Katika machapisho hayo, Kabba anahisi kwamba kitendo cha Ray kutumia gharama nyingi katika tafrija ya kudhihirisha jinsia ya mtoto wake ni kujighasi tu, lakini pia ni kuigiza maisha ambayo si yake halisi.

“Ni vizuri siku zote kuwa wewe mwenyewe halisi katika maisha yako. Usijaribu kuwaridhisha watu. Mimi hata sijali kuhusu wewe, kuwa halisi…. Usijaribu kuwa kama mtu mwingine, hakikisha unajiboresha mwenyewe,” Kabba aliandika kwenye instastory akiwa ameweka picha yake kwenye ufuo wa bahari.

Juzi pia, Kabba alipakia klipu ya mwanamke ambaye alikuwa anawapa mzomo watu ambao wanajaribu kuigiza maisha mitandaondi kwa kuwa nusu uchi, maudhui ambayo wengi walihisi Kabba alikuwa anamfuma Ray nayo.

Si mara ya kwanza ambapo Kabba anamfuma Amber Ray, baada ya kumaliza uhusiano wao ulidumu kwa wiki chache tu, Kabba aliandika Instagram akionesha kujuta kwake kumpenda Ray, jambo ambalo alisema kwamba kama angemjua ni mtu wa aina gani wala asingedhubutu kuingia kwenye mapenzi naye.

“Sidhani kila mtu anashangaa kwamba Amber Ray amesonga mbele na maisha. Ikiwa ningejua alikuwa mtu wa aina gani tangu mwanzo, nisingewahi kujihusisha naye. Sijutii tulichokuwa nacho, lakini inaonekana kwamba amehama mara nyingi hapo awali.”