Diana Marua afichua majuto yake baada ya kifo cha nyanya yake

Majuto yake ni kwamba alimkatisha tamaa wakati fulani na hilo ndilo lililomvunja moyo baada ya kifo chake.

Muhtasari
  • Diana aliongeza kuwa bibi yake aliaga dunia siku ile ile aliyopanga kumtembelea hospitalini.

Kwenye chaneli ya dadake ya YouTube inayoitwa 'Michelle Ngoje' Diana Bahati kwa mara ya kwanza alifunguka kuhusu kifo cha nyanyake na majuto yake.

Alifichua kwamba hakuwahi kutumia muda mwingi na nyanyake kama dadake mdogo Mitchelle.

Diana alieleza kwenye video hiyo kwamba kukabiliana na huzuni baada ya kifo chake haikuwa rahisi kwake kwa sababu wakati wowote akifumba macho angemwona nyanya yake.

"Shosho alikuwa akija akilini mwangu kila siku. Haikupita hata dakika tano baada ya kupita. Siku zote nilikuwa nikifunga macho yangu na kumuona nyanya yangu."

Majuto yake ni kwamba alimkatisha tamaa wakati fulani na hilo ndilo lililomvunja moyo baada ya kifo chake.

"Niseme tu ukweli nahisi nilimwangusha wakati fulani. Lakini sitazungumza juu yake. Nina sababu zangu. Nafikiri hiyo ndiyo sababu iliyonifanya kuumia zaidi na kuvunjika moyo zaidi. Mungu anajua. moyo wangu na popote ulipo Shosho mbinguni ukinitazama unajua moyo wangu na sasa unajua kwanini."

Diana aliongeza kuwa bibi yake aliaga dunia siku ile ile aliyopanga kumtembelea hospitalini.

“Niliambiwa anaumwa kidogo, nilitakiwa kwenda kumuona na watoto Jumapili ijayo, ilikuwa Jumatatu, nilirudi nyumbani nikihisi huyu si Shosho wangu, niliamua kwenda kufunga virago na kumuona. siku iliyofuata.Nilipojiandaa kwenda nilikuwa nimebeba begi langu la mkono nikiiwasha simu yangu nikienda kwenye gari, ujumbe wa kwanza ulikuwa ni ujumbe wa mjomba akiniambia 'Mama ametuacha'. Ooh my gosh!"