'Bilionea' KRG afichua jinsi alivyopata utajiri wake, na si kupitia muziki!

KRG anadai alipata zabuni ya kusambaza mchanga na kokoto kwa ujenzi wa reli ya SGR, na pia kurithi utajiri mkubwa wa nyanya yake.

Muhtasari

Mwaka wa 2007, nyanya yake kabla ya kufariki siku 30 kabla ya kuzaliwa kwa KRG, alitoa wosia kwamba mali yake yote ni ya KRG.

• Kati ya 2014 na 2016, msanii huyo alipata zabuni ya kusambaza mchanga na kokoto kwa ujenzi wa reli ya kisasa SGR.

KRG afichua chanzo cha utajiri wake.
KRG afichua chanzo cha utajiri wake.
Image: Instagram

‘Bilionea wa mchongo’ KRG The Don kwa mara ya kwanza amezungumzia kwa undani asili na chanzo cha utajiri wake huo mkubwa, licha ya kutotambulika pakubwa katika tasnia ya kimuziki.

Katika podikasti moja, msanii huyo aliweka wazi kwamba ni kweli yeye ni bilionea wala si utani kama ambavyo wengi wamekuwa wakimchukulia kila mara anaposema kuwa ni tajiri mkubwa mno nchini.

Msanii Krg, licha ya kutokuwa na mafanikio makubwa kimuziki, amekuwa akionekana akiteleza kwa magari mazito na ghali huku akila bati kwenye sehemu mbali mbali za kifahari, jambo ambalo limekuwa likizua maswali mengi kutoka baadhi ya wakenya kuhoji utajiri wake.

Alikuwa anasemekana kuwa ndiye mmiliki wa kilabu ya starehe iliyoko barabara ya Ngong, Casavera lakini fununu pia zikadai kwamba si yeye mmiliki halali, japo mwenyewe hajawahi lizungumzia hilo hadharani.

Lakini katika podikasti ile, KRG alisema kwamba utajiri wake ulianza tu mwezi mmoja alipozaliwa miaka mingi nyuma na ukaja kuongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka 2014.

Msanii huyo mwenye kujitapa sana alisema kwamab alirithishwa mali yote ya nyanya yake ambaye alifariki mwezi mmoja tu kabla ya kuzaliwa kwake na pia ilipofika mwana 2014, alipata zabuni ya kusambaza malighafi ya kujenga reli mpya ya kisasa, SGR kutoka ukambani hadi Nairobi – dili lililomuingizia mamilioni ya pesa na kumpaisha hadi kwenye ghrofa ya mabilionea.

“Nilianza maisha pole pole, nikakuta, kama hii kazi ya SGR, nilipata kazi yangu hapo. Tuliifanya hiyo kazi kutoka 2014 hadi 2016. Mimi nilikuwa nimepewa zabuni ya kuwaletea mchanga na kokoto kutoka huko Makindu hadi hapa, na hiyo yote ni mimi nimejenga,”         KRG alijipiga kifua.

“Kwa bahati mzuri tena huko nyuma, historia yangu mimi ndo kusema katika familia yangu yote. Hata baba yangu hawezi zungumza mbele yangu, wanatulia naongea kwanza ndio wanaongea. Kwa sababu urithi wa babu na bibi yangu wote ni mimi niliachiwa. Nyanya Alikufa siku 30 kabla nizaliwe na alikuwa amembariki mama yangu akisema yule mtoto atazaliwa ndiye mrithi wa hii mali, ambaye ni mimi sasa nilikuwa tumboni. Alifariki 2007 na kabla afariki aliita kila mtu akawaelezea kwamba ni mimi nitachukua kila kitu chake,” KRG aliongeza.