Maswali yaibuliwa 'paybill' ya Jeff Mwathi ikianzishwa licha ya kuzikwa wiki kadhaa zilizopita

"Kesi inayohusiana na mauaji na wakati jamhuri ndio mlalamishi haihitaji wakili, na Jeff alizikwa kitambo, sasa mchango ni wa nini?" Mmoja aliuliza.

Muhtasari

• Baadhi walihisi hakuna haja ya mchango wakati Jeff taayri alishazikwa na suala la uchunguzi likiwa mikononi mwa Serikali.

• Hata hivyo wengine walimpongeza Muthiora kwa kufanya kazi nzuri ya kuhakikisha familia ya Mwathi inapata haki.

Jeff Mwathi, aliyefariki kwa utata nyumbani kwa DJ Fatxo
Jeff Mwathi, aliyefariki kwa utata nyumbani kwa DJ Fatxo
Image: Facebook//Simon Mwangi Muthiora

Maswali chungu nzima yameibuliwa mitandaoni baada ya familia ya Jeff Mwathi, kijana aliyefariki kwa njia tatanishi nyumbani kwa DJ Fatxo kufungua pyabill ya mchango.

Mtetezi mkubwa wa kutaka haki itendeke, Simon Mwangi Muthiora alifichua habari hizo kupitia ukurasa wa Nairobian katika mtandao wa Telegram ambao anauendesha.

Alifichua kwamba hatimaye familia hiyo imefikia uamuzi wa kufungua paybill kwa ajili ya mchango wa kumsaidia, lakini watu mitandaoni walikuwa na maoni kinzani, haswa ikizingatiwa kwamba kijana huyo aliyefariki Februari 22 alizikwa kwa haraka mno kipindi hicho.

Wengi walionekana kushangazwa na hatua ya familia yake kufungua pyabill ya mchango licha ya kijana huyo kuzikwa na kuibua wasiwasi wao kwamba huenda suala la kifo cha Jeff limegeuzwa kuwa kitonga ambapo baadhi ya watu wanataka kujifaidi kutokana na kuenezwa kwa tanzia yake.

“Paybill ni ya nini tena? Najua mtanitusi lakini hii tabia ya kuchanga wakati mtu amefariki na kuzikwa ni upuzi. Kesi inayohusiana na mauaji na wakati jamhuri ndio mlalamishi haihitaji wakili,” David Bin Wan alisema.

“Mnachanga pesa za nini? Jeff tayari amezikwa, DCI wanafanya kazi yaoili kutumbua wahusika. Acha tuwe wakweli na tuelezeeni,” Oscar Kimani alisema.

“Wakati ninaona alama ya hatari huwa najitenga mbali, Kesi ya Jeff imecukuliwa na Jamhuri na mazishi yalishamalizika kwa hiyo sioni haja ya kuchanga hizi pesa, na kwa sababu hiyo, sihusiki katika hili, ila tuendeleze harakati ya haki kwa Jeff,” Lyrical Abdul alisema.

Muthiora hata hivyo aliruka kwa haraka kupitia ukurasa wake wa Facebook na kujitetea vikali akisema kwamba anajua watu hupenda kuwapaka wengine tope haswa ikifika ni mahali pesa zinahusika.

Alijisafisha na kusema kwamba yeye anaongoza harakati tu za kupatikana kwa haki ya marehemu Jeff na wala hamjui wala kumjua mtu yeyote kutoka kwa familia yake isipokuwa binamu yake Samidoh ambaye hata hivyo walikutana mwaka jana katika tamasha.

“Paybill inamilikiwa na mamake Jeff, watu waliomba kwamba afunguliwe. Mimi nilianza kumsaidia mamake Jeff hata kabla ya kumjua…. Tafadhali msinihusishe hapa kwa zogo la pesa, ni Zaidi ya haki kwa Jeff,” Muthiora alisema.