Si kwamba nilikukataa ila moyo wangu ulisita - Harmonize amuimbia Kajala kwa hisia

Harmonize alikuwa anaimba wimbo wa Belle 9 "Sumu ya Penzi" ambapo katika kibwagizo alipachika jina la Kajala.

Muhtasari

• Harmonize walirudiana na Kajala mwaka jana baada ya kutengana kwa zaidi ya miezi 10 vlakini miezi 6 tu ndani ya uhusiano mpya tena wakatengana.

Harmonize amkumbuka Kajala kwa wimbo wa Belle 9
Harmonize amkumbuka Kajala kwa wimbo wa Belle 9
Image: Instagram

Harmonize kwa mara nyingine tena ameonesha kwamba bado ana maruweruwe kutokana na kuachwa kwa ghafla na mwigizaji Kajala Masanja.

Wikendi iliyopita, msanii huyo alihudhuria na kutumbuiza kwenye tamasha la kampuni moja ya bia huko Mbeya, ambapo jukwaani alijumuika na msanii mmoja wa kitambo, Belle 9.

Akiwa jukwaani, aliimba wimbo maarufu wa Belle 9, ‘Sumu ya Penzi’ – wimbo ambao tunaweza sema kwamba ndio ulimtoa kabisa na kumtambulisha msanii huyo katika majukwaa makubwa ya Sanaa.

Harmonize aliimba wimbo huo neno baada ya linguine utadhani ni wake na katika kibwagizo chake, msanii huyo alipachika jina la Kajana akisema kwamba hakumkataa bali moyo wake ulisita.

“Sumu ya penzi nishailamba hata kwa maziwe siwezi kupona, sio kwamba nilikukataa, ila moyo wangu ulisita, wazazi wangu watanishangaa, nyumbani wewe ulishatoroka.. Kajala sio kwamba nilikukataa, ila moyo wangu ulisita…” Harmonize aliimba pamoja na mashabiki kwa mbwembwe.

Baada ya tukio hilo, Harmonize alimaliza akipiga magoti kwa kusujudu miguuni pa Belle 9 kama njia moja ya kumpa maua yake angali hai kwa kumpa msukumo wa kujiunga katika Sanaa ya muziki kipindi hajaanza kuimba.

Belle 9 kwa upande wake alijawa na furaha na kupakia video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kusema kwamba alijihisi kukoshwa na kiwango cha heshima aliyopewa na Harmonize.

Heshima hujificha katika upendo uliopo mioyoni mwa watu na sio wote wanaweza kuionyesha japo mara kadhaa nimeonyeshwa na inanipa moyo na nguvu yakuhisi ninachokifanya ni sahihi. Lakini ulichofanya @harmonize_tz hii ni kubwa sana kwangu, kwa mashabiki na familia yangu kutoka moyoni, ndugu yangu @harmonize_tz hii ni zaidi ya upendo, heshima na kila namna ya thamani,” Belle 9 aliandika kwa furaha.

Harmonize na Kajala walivishana pete za uchumba Juni mwaka jana lakini miezi 6 baadae kila mmoja aliondoka na hamsini zake kimya kimya bila kufunguka kiini kilichosababisha kutengana kwao wakati mashabiki walikuwa wanasubiria harusi.