Octopizzo: Kwa nini siwezi kuwasaidia wasanii tulioanza nao safari ya muziki Kibera

Marafiki zangu walinikasiria eti nimewakwepa, mimi si baba ya mtu. Tulipatana mtaani na nitaendelea. Wewe si ndugu yangu,” Octopizzo alisema.

Muhtasari

• Octopizzo alisema kama kuna msanii waliyeanza naye na anataka kufanya kazi naye, yeye hawezi jishusha chini bali ni huyo msanii apae hadi kumfikia kule juu.

Octopizzo, msanii wa muda mrefu wa rap
Octopizzo, msanii wa muda mrefu wa rap
Image: Instagram

Rapper wa muda mrefu kutoka mtaa duni wa Kibera, Octopizzo amezungumzia shutuma dhidi yake kuwa hajawahi wasaidia wasanii wa kutoka Kibera, haswa haswa wale ambao walianza safari ya muziki naye.

Octopizzo ambaye alikuwa anazungumza katika podikasti moja siku chache zilizopita alikiri kwamba ni kweli hajawahi wasaidia wasanii hao, lakini pia akautetea uamuzi wake kwa nini hafanyi hivo.

Octopizzo alisema kwamba ni ukweli ‘aliomoka’ kimaisha na kupaa ngazi za juu na hawezi kurudi chini kuwasaidia wenzake kwani yeye si mzazi wao.

Msanii huyo mwenye misimamo mikali katika maisha alisema kwamba wasanii ikiwa wanataka kufanya kazi naye ili awasaidie ni wajikakamue na kutia bidii ili kufika ngazi za juu aliko, lakini yeye hawezi kushuka chini ili kuwainua.

“Kuna wasanii wote walikuwa wanasema Octo wewe ndio kusema, niliwaambia mimi sipendi hiyo mbio unanipeleka, ukianza kunipeleka hivo utaniharibia biashara zangu, ni au uchague kubadilisha mienendo yako ukue hadi penye niko na mimi siwezi kuja hadi uko chini uliko. Mimi siwezi kuteremko,” Octopizzo alisema.

Rapa huyo alisema baadhi ya wasanii hao walioanza naye wengi wana chuki na yeye na hawajawahi mfikia uso kwa uso kumuambia kile ambacho hawapendi kumhusu, kwa sababu hajui mbona kuna chuki.

“Juzi hata nimesikia wamechukia albamu yangu yenye imetoka, nimewahi enda sehemu nikawapata lakini hawajawahi niambia niliwafanyia nini. Kama wewe ni rafiki unayesema mnoma si unakuja tu unaniambia mimi sipendi hivi.”

Octopizzo aliweka wazi kwamba yeye si msanii anayependa kufanya collabo na wasanii wengine, kwani anafanya uamuzi wake kivyake tu.

“Mimi si msanii wa kufanya collabo, hata ukuwe ndugu yangu mimi nitakuambia wewe fanya mambo yako mimi sitaki,” alisema.

Kuhusu ni kwa nini hawezi fanya muziki au kutumia maprodusa wa humu nchini, Octopizzo alisema kwamba alianza Kibera na hawezi kufanya muziki na midundo ya humu nchini kwani anataka kuionesha dunia kwamba naye amekua na ndio maana anatumia maprodusa wa ughaibuni.

“Mtu hufai kuchukia ukiona nimetoa ngoma na produsa wa nje, unafaa ufurahi kwa sababu nimekua hadi kufikia ngazi zile za juu. Marafiki zangu walinikasiria eti nimewakwepa, mimi si baba ya mtu. Tulipatana mtaani na nitaendelea. Wewe si ndugu yangu,” Octopizzo alisema.