Wawili waliojifunika blanketi moja achana nao kabisa: Rayvanny na Fahyvanny wamerudiana!

“Mtoto mbichi teketeke ak Mama umelainika. Umeumbika, acha nikumwagie sifa." Rayvanny alimwimbia Fahyvanny kwa mahaba baharini kwenye boti.

Muhtasari

• "Waruke sakara na mateke uzuri wako hawatofika, mama umejazisha, mikate ya kumiminisha….” Rayvanny anaimba kwenye wimbo huo.

Rayvanny na Fahyvanny wakioneshana mahaba mazito baharini kwenye boti.
Rayvanny na Fahyvanny wakioneshana mahaba mazito baharini kwenye boti.
Image: Screengrab//Instagram

Msanii Rayvanny ameachia video ya kibao kipya #Forever kutoka kwenye albamu yake ya Flowers III, mwezi mmoja baada ya kuachia pande la sauti la kibao hicho.

Video ya kibao hicho imekuja kama mshtuko kwa wengi, kwani msanii huyo bosi wa lebo ya Next Level Music ameamua kuwatia pamba mdomoni wambea waliokuwa wanasema kuwa hakuna maelewano baina yake na mzazi mwenzake, Fahyvanny.

Rayvanny amemshirikisha mama wa mtoto wake katika video hiyo kama Vixen na amempa makopa yote kwa mahaba mazito, kana kwamba mistari ya wimbo wenyewe kaitunga makusudi tu kwa minajili ya Fahyvanny.

“Mtoto mbichi teketeke ak Mama umelainika. Umeumbika, acha nikumwagie sifa. Waruke sakara na mateke uzuri wako hawatofika, mama umejazisha, mikate ya kumiminisha….” Rayvanny anaimba kwenye pande la video hiyo ambayo Fahyvanny mwenyewe aliipakia kwenye ukurasa wake wa Instagram kama kionjo cha video nzima iliyotoka mapema asubuhi ya Jumamosi.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza wawili hao kudokeza kuwa wamerudiana, japo ndio kama mara ya kwanza kabisa wanaibua mahaba yao hadharani, takribani miaka minne na miezi kadhaa baada ya kuachana.

Fahyvanny na Rayvanny walitengana mwaka wa 2019 kila mmoja akaamua kujishughulisha na hasmini za kwake, ambapo Rayvanny haikumchukua muda kabla ya kuzama kwenye huba zito na mrembo wa mwigizaji Kajala Fridah, Paula.

Hata hivyo, Paula na Rayvanny mwaka jana walidokeza kuwa wametengana na Rayvanny katika mahojiano kipindi hicho alipotakiwa kuchagua baina ya Paula na Fahyvanny, alisitia kidogo lakini kwa ishara zote akaonekana kuegemea kwa yule ambaye ana mtoto wake – Fahyvanny.

Tangia haoi kumekuwa na fununu za chini kwa chini kuwa wamerudiana, baadhi wakiibua kurudiana tena na Paula lakini safari hii wameamua kuficha kumetosha na wamekuja hadharani kabisa kwenye pande la video ya mahaba #Forever.