Kaa mbali na biashara zangu, acha kunitaja kila wakati - Stevo amuonya Pritty Vishy

Stevo alishangaa kama ma ex wengine pia hufanya hivyo kwa wapenzi wa zamani ama tukio hilo linamtokea yeye tu na uzuri wake.

Muhtasari

• Pritty Vishy amekuwa akitoa maoni yake katika kila kitu ambacho Stevo Simple Boy anahusishwa kufanya, kutoka kwa ngoma hadi mpenzi mpya.

• Mapema mwezi huu Stevo aliposema mpenzi wake ana mimba, Vishy alikuwa mtu wa kwanza kudai kwamba mimba hiyo si ya Stevo.

Stevo amtaka Vishy kukoma kumtajataja kila wakati
Stevo amtaka Vishy kukoma kumtajataja kila wakati
Image: Instagram

Kwa mara nyingine tena msanii mpole Stevo Simple Boy amevunja upole wake na kumkoromea vikali aliyekuwa mpenzi wake, mwanablogu Pritty Vishy na kumtaka kukaa mbali na mambo yake.

Stevo kupitia ujumbe huo wa onyo alioandika kwenye instastory yake, alimtaka Vishy kuheshima ukweli kwamba walisha achana na ni muda sasa kila mmoja kujishughulisha na hamsini za kwake.

Alimwambia Vishy kulitema kabisa jina lake kutoka kwa mdomo wake na kukoma kuzungumzia mambo yoyote yanayomhusu, huku pia akishangaa kama wapenzi wa zamani wako hivo kwa watu wengine.

“Ex kaa mbali na kando jamani. Wachana na biashara zangu kabisa. Si lazima unitaje kila saa, duuh, sijui kama ma ex zenu pia wako hivi,” Stevo Simple Boy aliwauliza mashabiki wake.

Pritty Vishy amekuwa akitoa maoni yake katika kila kitu ambacho Stevo Simple Boy anahusishwa kufanya, kutoka kwa ngoma hadi mpenzi mpya.

Mapema mwezi huu baada ya Stevo kudai kwamba mpenzi wake mpya Grace ni mjamzito, Vishy alikuwa wa kwanza kuruka mitandaoni akisema kuwa mimba hiyo si ya Stevo, lakini baadae Stevo akabainisha kwamba alikuwa anawatania mashabiki zake siku ya wajinga ya Aprili mosi.

Katika kila itu ambacho Vishy anafanya mitandaoni, kwa namna moja au nyingine utampata akimtaja Stevo ambaye waliachana mapema mwaka jana.

Baadhi ya watu wamekuwa wakihisi kwamba mwanadada huyo bado anamhitaji sana Stevo katika maisha yake kwani si kawaida kwa mtu kuendelea kumtaja mtu ambaye mlishatengana na mpaka kila mmoja kusonga mbele na harakati zake za kimaisha.