Nakupenda tu, wewe ni mwanamume mzuri - Karen Nyamu amwambia Jimal Rohosafi

Nyamu alisema kuwa mke wa kwanza hafai kuvunja ndoa na mume wake kwa sababu ya kupata mke wa pili, akimlenga Amira.

Muhtasari

• Nyamu alimshauri Jimal endapo Amira atarudi - jambo ambalo alisema ana imani nalo - basi awasawazishe wote na Amber Ray.

• Jimal wamekuwa wakionekana na Amber Ray baada ya mwanamitindo huyo kuachana na Rapudo licha ya kuwa na mimba yake.

Karen Nyamu amwambia Jimal anampenda, ampa ushauri kuhusu ndoa ya wake wawili.
Karen Nyamu amwambia Jimal anampenda, ampa ushauri kuhusu ndoa ya wake wawili.
Image: Instagram

Seneta mteule Karen Nyamu kwa mara nyingine tena amekuwa gumzo la mitandao ya kijamii baada ya kuibuka na mapya, safari hii akizungumzia maisha ya kimapenzi kati ya mfanyibiashara Jimal Rohosafi na mke wake wa kwanza Amira na mpenzi Amber Ray.

Ilianza pale Jimal alipopakia picha ya mguu wa mtoto akiwa amekanyaga juu ya mguu wa mtu mzima na kusema kwamba katika maisha kitu kinachompa baba furaha na fahari kubwa ni kuhisi uwepo wa mikono ya binti yake kwenye shingo lake.

“Vito vya thamani zaidi, utawahi kuwa karibu na shingo yaambavyo vinaweza kuzunguka shingo lako, ni mikono ya binti yako,” Jimal alisema.

Nyamu kwenye maoni alimwandikia Jimal ujumbe ambao umeibua gumzo kwa mara nyingine tena, akimwambia kuwa anampenda sana na kuzama ndani Zaidi kuzungumzia ndoa yake iliyovunjika na Amira.

“Jimal nakupenda tu, wewe ni mwanamume mzuri,” Nyamu alisema.

Seneta huyo ambaye amekuwa akisutwa kwa ‘kufanya ndoa ya Samidoh na Edday kuingiwa na misukosuko’ aliendelea kusema kwamba Amira alifanya makosa makubwa sana kumuacha kisa amepata mwanamke mwingine – Amber Ray.

Kulingana na Nyamu, mke wa kwanza hafai kuvunja ndoa yake ya kwanza kwa sababu mume wake amepata mke wa pili.

Nyamu alisema kuwa ana Imani siku moja Amira atarudi kwenye ndoa yake na kumshauri Jimal kuwa atumie kigezo cha kuwasawazisha kwani ndio ufunguo wa ufanisi wa ndoa ya mitala.

“Kama vile nilivyokuambia kila mara, Amira alifanya makosa kukuacha kwa sababu ya mwanamke mwingine. Natumai siku moja atarudi unawaweza wote, kuwasawazisha ndio ufunguo wa kuwamudu,” Nyamu alitema lulu.

Baadhi walitafsiri ujumbe huu kwa maana tofauti, wakisema kuwa ndio ushauri wa moja kwa moja aliokuwa pia akiutuma kwa mke mwenza, Edday Nderitu ambaye amekuwa akitishia kuvunja ndoa yake ya miaka 15 na mwanamuziki Samidoh kwa kumpenda Karen Nyamu kama mke wa pili.

Samidoh, afisa wa polisi ambaye pia ni msanii wa Mugithi amekuwa akigonga vichwa vya habari kufuatia vimbwanga baina ya Edday Nderitu na Karen Nyamu ambao wote wamezaa naye watoto.