Mr Seed anusurika katika ajali mbaya ya barabarani iliyogharimu maisha ya wenzake

Mkewe alisema kuwa mumewe alikuwa katika gari na wenzake ambao walifariki lakini yeye na baadhi ya wengine walinusurika na wako hospitalini.

Muhtasari

• “Siamini kama  mume wangu yuko hai. Sijawahi patwa na wasiwasi kama huu maishani mwangu." - Nimo alisema.

Mr Seed ahusika katika ajali mbaya ya barabarani.
Mr Seed ahusika katika ajali mbaya ya barabarani.
Image: Instagram

Msanii Mr Seed Jumamos alihusika katika ajali mbaya ya barabarani kulingana na taarifa kutoka kwa mke wake Nimo Gachuiri.

Kulingana na taarifs zilizopo, Mr Seed alikuwa kwenye gari na baadhi ya marafiki zake akiwemo msanii mwenzake wa injili DK Kwenye Beat.

Nimo ambaye alipakia msururu wa picha na video kwenye instastories zake alisema kuwa hajawahi pata woga kama ambavyo alipata wakati huo na ilihitaji wasamaria wema kufika ili kuwakimbiza majeruhi hospitalini.

Nimo alisema kuwa alikuwa anachukua video hizo kuwataarifu wanafamilia na kusema kuwa kutokana na kilichotokea, atakuwa nje ya mitandao ya kijamii kwa muda.

“Siamini kama  mume wangu yuko hai. Sijawahi patwa na wasiwasi kama huu maishani mwangu. Wasamaria wema walinisaidia na tulimkimbiza hospitalini. Nilikuwa nachukua video hizi kwa ajili ya wanafamilia,” Nimo alisema.

Alisimulia kwamba gari ambalo mumewe alikuwa ndani lilikuwa mbele ya lile ambalo yeye alikuwa anasafiria na walipigwa na butwaa walipoona watu wamejazana na kufika wakapata na mumewe na wenzake wamepata ajali.

"Nakumbuka tu nilikimbia na kuwaona chini na kumwomba waamke. Sijui kama niwe na furaha kwamba baadhi ya marafiki walisalimika katika ajali hiyo kwa sababu pia siwezi kosa kulia kuwa baadhi walipoteza maisha,” Nimo alisema.

Nimo alisema kuwa alichokiona si tofauti na muujiza kwani mume wake yuko hai hata ingawa ana maumivu makali kutokana na majeraha aliyoyapata.

“Seed ako sawa hata ingawa ana maumivu kwenye nyonga. Ameagizwa kuwa kitandani kwa wiki mbili. Tuombeeni na pia zile familia za wale ambao kwa bahati mbaya walifariki,” Nimo aliandika.