Alikiba aitambua ngoma ya Diamond katika kusherehekea chimbuko la Bongo Flava

Alikiba aliteuliwa kuwakilisha simulizi la chimbuko la muziki wa Bongo Fleva ambao ulianza miaka ya 1990s na ambao unatoa ladha kamili ya tamaduni za Afrika Mashariki.

Muhtasari

• Miezi michache iliyopita Diamond pia aliitambua ngoma ya Alikiba kama pendwa kwake.

• Muziki wa Bongo Fleva unatoa ladha, hisia na uhalisia kamili wa tamaduni za ukanda wa Afrika Mashariki.

Alikiba aikubali ngoma ya Diamond kwenye chimbuko la Bongo Flava.
Alikiba aikubali ngoma ya Diamond kwenye chimbuko la Bongo Flava.
Image: Instagram

Jukwaa la kusambaza miziki kwa njia ya kidijitali, Apple Music limezindua kipengele cha kusherehekea chimbuko la miziki ya Kiafrika katika mwezi huu wa Mei.

Kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, Apple Music walimteua msanii mwenye mafanikio mengi katika muziki wa Bongo Flava, Alikiba kutoka lebo ya Kings Music.

Katika uteuzi huo, msanii anatakiwa kutoa historia ya muziki anaouwakilisha wa Kiafrika na pia kutaja baadhi ya nyimbo ambazo anahisi zinamkosha na kuleta ladha na uhalisia kamili wa muziki huo.

“Mwezi wa Mei tunasherehekea AFRICA MONTH, ungana na Alikiba & @applemusic kusherehekea CHIMBUKO cha Bongo fleva, huku tukisimulia chimbuko la aina ya muziki wetu na mchango wake kwenye muziki wa kisasa, kwa upendo nilisimamia orodha yangu ya kucheza "Alikiba" (Bongo Fleva Origins) kuuruhusu ulimwengu kusikiliza nyimbo chache zinazowakilisha muziki wetu. Furahia,” Alikiba alisema.

Msanii huyo aliandaa orodha ya ngoma nyingi tu zenye ladha ya Bongo Flava ambazo kwake zinaleta hisia, ladha na uhalisia kamili wa aina hiyo ya muziki ambayo kwa Zaidi ya miaka 30 imekuwa ikibeba maana halisi ya utamaduni wa Afrika Mashariki.

Kilichowashangaza wengi ni pale ambapo Alikiba aliitaja ngoma ya hasidi wake wa muda mrefu katika Sanaa ya muziki, Diamond Platnumz kuwa moja ya ngoma zake pendwa na ambazo zinatoa ladha kamili ya Bongo Flava.

African Beauty – ngoma ya Diamond ambayo alimshirikisha Omarion kutoka Nigeria katika albamu yake ya Boy From Tandale ndio ngoma ambayo Alikiba aliipigia saluti.

Kando na ngoma ya Diamond, msanii huyo pia aliteua ngoma za wasanii wanaoshindana nao kama Marioo na Harmonize kweney orodha yake huku wengine wengi wakiwa ni wasanii wa lebo yake ya Kings Music akiwemo kakake Abdukiba, Vanilla na wengine.

Gumzo kubwa lilijikita kwa ngoma ya Diamond ambayo licha ya uhasama uliopo baina yao, Alikiba alionesha kwamba ni mfuatiliaji mkubwa wa kazi za msanii mwenzake.

Miezi michache iliyopita msanii Diamond pia kupitia instastory yake alipakia ngoma ya Alikiba, Asali na kusema kuwa ni moja ya ngoma anazozikubali sana kutoka kwa mwamba huyo wa mrengo pinzani kimuziki.