Diamond: Kwa nini niliamua kucheza kama 'video king' kwa wimbo mpya wa Zuchu

Diamond alisema kuwa Zuchu hakumlipa hata senti moja kushiriki kama video king kwenye wimbo wake wa Utaniua.

Muhtasari

• "Niliona sio mbaya mimi kucheza kama video king kwa sababu italeta kitu tofauti na utamu kwenye nyimbo Zaidi." - Diamond.

Diamond Platnumz afichua kwa nini alishiriki kwenye video ya Zuchu.
Diamond Platnumz afichua kwa nini alishiriki kwenye video ya Zuchu.
Image: Screengrab//Zuchu

Baada ya kusakamwa na wengi wakimtaka kujitetea ni kwa nini alishiriki kama ‘video king’ kwenye wimbo mpya wa Zuchu – Utaniua, hatimaye Diamond Platnumz amevunja kimya chake.

Diamond katika mahojiano kwa njia ya simu na kituo cha redio cha Wasafi FM, alikiri kwamba alichangia pakubwa katika kupamba video ya Zuchu na kufichua kwamba hakulipwa hata senti kucheza kama ‘video king’.

“Zuchu ni msanii wangu tunafanya kazi pamoja na jukumu langu ni kuhakikisha kwamba nawekeza nguvu zangu ili mambo yake yaende. Niliona sio mbaya mimi kucheza kama video king kwa sababu italeta kitu tofauti na utamu kwenye nyimbo Zaidi. Sijalipwa lakini unajua nikiwa kama kiongozi katika taasisi na yule ni miongoni mwa watu ambao tunafanya kazi pamoja,” Diamond alisema.

 Msanii huyo pia alisema kuwa ilikuwa rahisi kwake kushiriki kama video king katika baadhi ya matukio kwa sababu alikuwepo tangia mwanzo wakati hadithi na maudhui ya wmbo yalikuwa yanatungwa na kuongozwa.

“Sikuwa na namna ya kukataa na singeweza kukataa kwa kweli,” Diamond alisema.

Diamond alitaja tukio moja ambalo lilimpa ugumu na ukakasi kushiriki kama video king ni pale wakiwa kwenye mvua ambapo ilibidi wakumbatiane na kuoneshana mahaba licha ya kuwa si wapenzi – awali mama Dangote alishaweka wazi kuhusu hili.

“Ki ukweli scene ya kwenye mvua pale, unajua sasa inabidi muonekane kama mnakumbatiana, ilileta ukakasi kidogo na ilinipa shida kwenye kushoot pale. Namna ambavyo mnatakiwa muonesha kama mna mahaba na nguo zishalowa kwa mvua inakuwa mushkil wallahi,” Diamond alisema.

Diamond pia alisema Zuchu alifanya video hiyo kitambo sana miezi miwili hivi nyuma kabla ya Ramadan.