Mama Dangote: Diamond hakuwahi toka kimapenzi na Zuchu, ilikuwa kuchangamsha genge tu!

Kwa wakati mmoja 2022, Diamond na Zuchu waliwaaminisha watu kuwa wangefunga harusi siku ya wapendanao wa Februari 14 mwaka huo.

Muhtasari

• Suala la mapenzi baina ya Diamond na Zuchu limeibuka tena baada ya wawili hao kuonekana kwenye wimbo wa Zuchu wakikumbatiana.

• Katika video hiyo, Diamond ndiye alishiriki kama mcheza video mkuu aliyebeba maana nzima ya wimbo wa Utaniua.

Mama Dangote akanusha Diamond kutoka kimapenzi na Zuchu.
Mama Dangote akanusha Diamond kutoka kimapenzi na Zuchu.
Image: Screengrab//YouTube

Mama Dangote kwa mara ya kwanza amezungumzia ukweli uliopo kwa kile ambacho kwa Zaidi ya mwaka mmoja kimekuwa kikitajwa kuwa mwanawe Diamond anatoka kimapenzi na Zuchu.

Mama Dangote alilazimika kunyoosha maelezo kuhusu sekeseke hizi ambazo zimekolezwa munyu kwa Zaidi ya mwaka mmoja kuhusu uhusiano wa Zuchu na bosi wake, pindi baada ya Diamond kuonekana akiigiza kama mbeba maudhui mkuu kwenye video ya wimbo mpya wa Zuchu, Utaniua.

Hii ndio mara ya kwanza kwa Diamond kuigiza kwenye video ya wimbo ambao hajashirikishwa na baadhi ya maudhui kwenye wimbo huo ni ya kimapenzi ambayo Diamond aliigiza barabara kama mhibu wa Zuchu.

Matukio hayo kwa mara nyingine yaliotesha uvumi wa wawili hao kuwa katika mapenzi kwani njia ambazo wanakumbatiana katika sehemu moja wakiwa wamelowa kwa kunyeshewa inaashiria mahaba na upendo wa kweli.

Lakini Mama Dangote alikanusha vikali hilo pia akisisitiza kwamba mwanawe Diamond hajawahi kuwa katika uhusiano wa mapenzi na Zuchu bali ni biashara tu na ili kunogesha biashara ya kimuziki, ilibidi ‘wachangamshe genge’ kwa kuigiza huba.

“Hakukuwa na mahusiano. Tulikuwa tunachangamsha genge tu ili tutrend,” Mama Dangote alipasua mbarika ya kille ambacho kwa muda mrefu baadhi walikuwa wanakisia kuwa Diamond na Zuchu si wapenzi bali ni kiki tu.

Miezi michache iliyopita, baada ya kushindwa tena kwendelea na wimbi la kuhusishwa kimapenzi, Zuchu akiweka taarifa kwamba uhusiano wake na Diamond umekwisha na kutangaza kuwa singo.