Hakuna aibu kabisa kufanya kazi za mjengo kujilisha mwenyewe na wapendwa wako - Dkt Mutua

Mutua alikuwa akizungumzia sakata la msanii Colonel Mustafa ambaye alionekana kweney video akifanya mjengo, aliomba namba yake kumpa msaada.

Muhtasari

• Mutua alisema kuwa hakuna tatizo kwa mtu kujibidiisha katika kazi ya mjengo ili kujilisha huku pia akifutilia mbali dhana kwamba kazi hizo ni za watu waliofeli maishani.

• “Lakini inahitaji ujasiri kwa mtu mashuhuri wa aina ya Mustafa kuchukua shughuli hizo duni kwa fahari." - Mutua.

Mutua amsifia pakubwa Colonel Mustafa kwa kutojihurumia na kuchagua kufanya kazi za mjengo.
Mutua amsifia pakubwa Colonel Mustafa kwa kutojihurumia na kuchagua kufanya kazi za mjengo.
Image: Instageam

Wiki jana, video ilienezwa mitandaoni ikimuonesha msanii wa muda mrefu Colonel Mustafa akishirikia kazi ya mjengo.

Video hiyo iliwavunja moyo sana baadhi ya Wakenya na mashabiki wake ambao walihuzunika kwamba baada ya miaka mingi ya kuwapa burudani, msanii huyo bado anahangaika maishani.

Wasanii wenza walijikusanya na kumfikia kwa msaada wa chochote kitu na kushauri aanzishe akaunti ya kutumiwa michango, haswa baada ya kukiri kwamba alilazimika kujihusisha na kazi za mjengo ili kujilisha na pia kumshughulikia mamake ambaye anaugua saratani, kimatibabu.

Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki ya wanamuziki nchini Kenya Dkt Ezekiel Mutua naye ameingilia kati suala hilo ambalo ameanza kwa kumtaka yeyote aliye na namba ya Mustafa kumpa.

Mutua alimshabikia Mustafa pakubwa akisema kuwa ni moja kati ya wasanii ambao licha ya maisha kuwaendea mrama, hakutebwereka tu na kujihurumia bali aliamua liwe liwalo ni sharti achakarike ili wanaomtegemea wapate kuishi vizuri.

Mutua alisema kuwa hakuna tatizo kwa mtu kujibidiisha katika kazi ya mjengo ili kujilisha huku pia akifutilia mbali dhana kwamba kazi hizo ni za watu waliofeli maishani.

“Mtu tafadhali inbox namba ya Mustafa. Nina upendo wa dhati na heshima kwa watu ambao wanakabiliwa na maisha na kufanya kile ambacho mwanaume anapaswa kufanya ili kuweka chakula mezani,” Mutua alisema.

“Hakuna aibu kabisa kuchukua mradi wa mjengo kujilisha mwenyewe na wapendwa. Tofauti na mastaa wengine, Mustafa amekataa kujionea huruma na haoni aibu na kazi zake. Na kwa njia, mjengo sio eti ni kazi kwa waliofeli. Ni kazi kama kazi nyingine yoyote,” Mutua aliongeza.

Mkurugenzi huyo alimsifia Mustafa kuwa ni wasanii wachache mno wanaoweza kukumbatia kazi kama hizo tena kwa kuzifurahia na kuzitapa bila kutazama jamii itawachukulia kwa njia gani.

“Lakini inahitaji ujasiri kwa mtu mashuhuri wa aina ya Mustafa kuchukua shughuli hizo duni kwa fahari. Ninapenda mtazamo chanya. Hii ndio aina ya kuungwa mkono,” Mutua alimaliza.