Colonel Mustafa alizwa na alichofanyiwa na bosi wa MCSK Ezekiel Mutua

Mutua aliapa kuhakikisha Mustafa anaanza kulipwa kwa nyimbo zake za zamani kuchezwa kwenye vyombo vya habari na kwenye matamasha, tafrija.

Muhtasari

• Alisema tayari amejitolea kumlipia Mustafa ada ya kujiunga na MCSK ambacho ni chama cha hakimiliki kwa kazi za sanaa.

Mutua kumlipia Mustafa ada ya kujiunga MCSK.
Mutua kumlipia Mustafa ada ya kujiunga MCSK.
Image: Facebook, Maktaba

Jumanne mkurugenzi mkuu wa MCSK Dkt Ezekiel Mutua alitoa ombi kwa yeyote aliye na namba ya rapa Colonel Mustafa ili kufanya mazungumzo naye.

Baadae, Mutua alirudi tena mitandaoni na kuweka wazi kwamba alifanikiwa kuzungumza na Mustafa kwa mapana na marefu na alifurahi kusikia sauti ya kidume mkakamavu licha ya kupitia madhira si haba katika kumuuguza mamake mgonjwa wa saratani.

Mutua alisema alikoshwa na ukweli na uaminifu wa Mustafa ambaye alikiri kuwa hajawahi kuwa mwanachama wa MCSK na kuahidi kumlipia ada ya kujisajili kama msanii mwanachama.

"Siwezi kungoja kuona talanta hii nzuri tena kwenye studio. Yeye sio mtu wa mjengo jamani. Ni mwanamuziki mwenye kipawa na nimejitolea kumlipia ili ajiunge na MCSK na kurejea kwenye muziki,” alisema kwa sehemu.

Kitendo hicho kulingana na Mutua kilimliza Mustafa ambaye amepata michango si haba kutoka kwa wahisani wema, wiki moja tu baada ya video yake kuenezwa akionekana kuchakaa katika kazi za mjengo ili kuhangaikia matibabu ya mamake.

Mutua pia aliahidi kumtafutia mawakili wazuri ili kuhakikisha kwamba anapata njia ya kulipwa kutokana na nyimbo zake za zamani kupigwa kwenye vyombo vya habari na kumbi za starehe.

“Pia tunawashirikisha wanasheria ili kuona jinsi gani anaweza kulipwa fidia kwa matumizi ya muziki wake na watangazaji na kwenye hafla za hadhara. Hakimiliki hutumika katika maisha yote na miaka 50 baada ya kifo. Nina hakika kuna wanasheria wazuri ambao wanaweza kusaidia kufuatilia mtazamo huu na kumsaidia Mustafa,” aliongeza.

 Awali, Mutua alimsifia Mustafa pakubwa akisema kuwa msanii huyo baada ya kupigwa dafrau na maisha, hakubaki chini bali alijizoa na kutafuta njia mbadala ya kukabiliana nayo.

Alisema kuwa wasanii wengi baada ya kuharibikiwa na mambo hayo hujichukia na kujificha lakini Mustafa hakujali hilo na hakutaka kuhurumiwa bali alijitoa mazima kwenda kutafuta kazi ngumu za mikono kuhakikisha kwamba mambo yake yanaenda.