• "Siitishi mtu pesa ya kujisajili au ya kitu chochote, msaada kutoka kwa Sonko ni bure bila ada yoyote kwa umma,” Sonko alisema.
Mhisani na mwanasiasa Mike Sonko siku moja baada ya video yake akijigamba na pesa nyingi kuenezwa, amesema kuwa yeye huwa hatozi kiasi chochote cha ada ili kutoa msaada kwa mtu yeyote mweye uhitaji.
Sonko alipakia video kwenye kurasa zake mitandaoni akiwatahadharisha umma kwamba kuna watu wamejitokeza wakitumia jina lake na kudai kwamba wanatoa misaada ya kifedha kwa watu wenye uhitaji kumbe ni walaghai.
Sonko alisema kuwa atakuwa anatoa tahadhari hiyo kila siku ili kuwaokoa watu ambao wamekuwa wakilalamika kulaghaiwa pesa na watu wanaojihusisha na yeye.
Mwanasiasa huyo mwenye mazoea ya kutoa msaada kwa watu wenye uhitaji mbalimbali alisema kuwa msaada wake yeye hutoa bila kuitisha hongo yoyote.
“Usitume pesa kwa pikipiki, hakuna pikipiki mimi napatiana. Kama ni kusaidia huwa nasaida bure. Siitishi mtu pesa ya kujisajili au ya kitu chochote, msaada kutoka kwa Sonko ni bure bila ada yoyote kwa umma,” Sonko alisema.
Sonko alifichua kwamba walaghai hao wamefikia hatua nyingine ya kuwaajiri wasichana kujifanya ndio makatibu katika ofisi ya Sonko ili kuitisha pesa kutoka kwa watu wenye uhitaji kabla ya kupokea msaada, kumbe ndio mwanzo wanafyonza kile kidogo walichobaki nacho.
Sonko amejitokeza kuzungumzia maswala ya pesa siku moja baada ya kuonekana akijigamba na pesa zake nyingi ambapo ilikisiwa alikuwa anamjibu jamaa mmoja aliyemghasi.
Kwenye video hiyo, Sonko alisikika akijigamba kwamba shilingi milioni mbili taslimu za Kenya alizokuwa nazo ni kidogo kwake kwani ni kama hela za mfukoni tu kwa ajili ya matumizi madogo kama kuweka gari lake mafuta.