Kamwe usimpe mwanaume jukwaa la kukukosea heshima - Akothee awashauri kina dada

"Wanawake wengi wamevunjika na kuharibiwa na uhusiano ambao haufai uwekezaji wao,” Akothee alitema lulu.

Muhtasari

• Akothee alishauri kina dada kutonyongonyea mbele ya wanaume ambao wanawaonesha madharau hadharani.

• Msanii huyo mama wa watoto watano alisema mwanamke anayejitambua hawezi kuvumilia manyanyaso kisa ndoa.

Akothee atoa ushauri kwa wanawake wanaonyanyasika kwenye ndoa
Akothee atoa ushauri kwa wanawake wanaonyanyasika kwenye ndoa
Image: Instagram

Mjasiriamali na mwanamuziki Akothee ambaye kwa muda mrefu alikuwa akijitambulisha kama rais wa kina mama wasio na waume kabla ya kuolewa mwezi jana amerudi tena safari hii akitoa ushauri kwa wanawake wote.

Mama huyo wa tambo nyingi aliwashauri wanawake kutoruhusu hata chembe ya muda na nafasi zao kuwapa wanaume ili kuwapaka dharau.

Akothee aliwataka kina mama kuweka mipaka ya kinachofanywa dhidi yao na kisichostahili ufanywa dhidi yao kuanzia mwanzo kabla mapenzi hayajakolea munyu.

“Kamwe usimpe mwanaume jukwaa la kukukosea heshima. Weka mambo sawa tangu mwanzo mjulishe cha kufanya na kisichofanywa. Wanawake wengi wamevunjika na kuharibiwa na uhusiano ambao haufai uwekezaji wao,” Akothee alitema lulu.

Msanii huyo mama wa watoto watano alisema kuwa hata kama mwanamke umeishi na mwanaume kwa miaka mingi ukiwa na matumaini kwamba atabadilika na haoneshi dalili zozote za kubadilika, usiendelee kuharibu muda wako badala yake jitoe na kuanza maisha yako binafsi.

“Ndio, labda mmeishi pamoja kwa miaka mingi, lakini Madam, Madam, ikiwa miaka ambayo umejitolea kufikiria kuwa anaweza kubadilika haimwongezi pia. Piga hatua, miliki maisha yako na uendelee. Wanadamu wanaweza kuwa wabinafsi sana. Usife mke mwaminifu na maisha matupu,” Akothee alisema.

 Hata hivyo, kabla ya kuzingatia ushauri huu wa Akothee, msanii huyo alitoa tahadhari kubwa akisema kuwa katika harakati za kutoka katika ndoa, mwanzo hakikisha kuwa utakwenda kuhangaika na lazima uwe na pesa zako.

“Lakini kwanza jitayarishe kuchakarika na upate uhuru wa kifedha. Wanawake wengi hawajastahiki Sanaa ya UPATIKANAJI, UDHIBITI NA UMILIKI,” Akothee alimaliza.