Arap Uria kuendesha baiskeli kutoka Eldoret hadi Nairobi Chelsea wakipepetwa na United

Mcheshi huyo shabiki maarufu wa Chelsea alikuwa ameahidi kabla ya mechi kuwa angeendesha baiskeli kwa 311KM kati ya Eldoret na Nairobi endapo United wangeinyuka Chelsea.

Muhtasari

• Eldoret hadi Nairobi ni umbali wa kilomita 311 ukipitia jiji la Nakuru na kilomita 390 ukitumia barabara ya Maai Mahiu-Narok.

• Uria ni shabiki sugu wa Chelsea ambaye alijizolea umaarufu kutokana na klipu zake akimuiga Peter Drury katika kutangaza mpira.

Arap Uria kuendesha baiskeli kilomita 311 kutoka Eldoret hadi Nairobi baada ya ubashiri wake kunywa maji katika mechi ya United na Chelsea.
Arap Uria kuendesha baiskeli kilomita 311 kutoka Eldoret hadi Nairobi baada ya ubashiri wake kunywa maji katika mechi ya United na Chelsea.
Image: Facebook//Arap Uria

Arap Uria, Mchekehsaji maarufu wa nchini Kenya ambaye alijizolea umaarufu kutokana na skits zake akimuiga mtangazaji wa kandanda Peter Drury, amelazimika kufanya kibarua kigumu maishani mwake baada ya ubashiri wake wa mechi kuenda mvange.

Alhamisi mchana kabla ya mechi ya ligi kuu baina ya Manchester United na Chelsea, shabiki huyo shakiki wa Chelsea alijitokeza na bango kubwa akidai kwamba alikuwa radhi kabisa kuendesha baiskeli kutoka mji wa Eldoret hadi jijini Nairobi – umbali wa kilomita 311- endapo United wangeipiga Chelsea au hata kupata sare.

“Nitaendesha baiskeli kutoka Eldoret hadi Nairobi ikiwa Manchester United watashinda au kutoka sare na Chelsea,” bango la Uria lilisoma huku akiwa amevalia sare za The Blues.

Kwa bahati mbaya upande wake, United waliinyuka Chelsea mabao 4-1 ugani Old Trafford, matokeo ambayo yalimaanisha kwamba Uria angetekeleza wajibu wa kuendesha basikeli umbali huo wote bila shuruti.

Wengi walidhani mcheshi huyo angebatilisha msimamo wake lakini hakuwa na jinsi kwani tayari maji alishayafulia, ilibidi ayakoge tu.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Uria alidokeza kwamba angeanza safari yake ya kutimiza kile alichokiahidi, huku akionekana tayari na kibaiskeli chake.

“Ni sawa hongera Man United. Safari yangu itaanza kesho na pengine nitawasili Nairobi Jumatatu. Nitahitaji maji njiani. Safari yangu ya kwenda Nairobi itaanza Zion mall Eldoret saa tisa asubuhi. Niletee maji na vichangamshi,” Uria aliandika.

Katika mechi hiyo, Ushindi kwa United uliwaweka katika nafasi ya tatu  na kuwahakikishia nafasi yao katika mabano nan ne bora kumaanisha kwamba msimu ujao watashiriki katika mashindano ya ligi ya mabingwa Ulaya.