Pasta wako hawezi kuwa babako au mamako - Ezekiel Mutua akubaliana na pasta Kiamah

“Uzushi huu lazima urekebishwe ili kuondoa upuuzi kanisani na kurejesha utulivu katika jamii,” Mutua alikemea.

Muhtasari

• Alisema kuwa wachungaji wengine wanafanya makusudi kutaka waitwe baba au mama kwa sababu wanajua kuwa neno la mzazi halina ubishi.

• Kulingana na Mutua, kumuita mchungaji baba au mama ni kuwakosea heshima wazazi waliokuzaa.

Ezekiel Mutua akubaliana na kauli ya mchungaji Tony Kiamah kuwa wachungaji hawafai kuitwa wazazi kwa waumini.
Ezekiel Mutua akubaliana na kauli ya mchungaji Tony Kiamah kuwa wachungaji hawafai kuitwa wazazi kwa waumini.
Image: Facebook

Wikendi iliyopita, video ya mchungaji wa kanisa la KAG Rivers of God, Tony Kiamah akihubiri kuwa mchungaji wa kanisa lako hafai kuwa mzazi wako ilienezwa mitandaonic ikivutia maoni mseto.

Kiamah aliwasuta wahubiri wengi ambao wanawataka waumini wao kuwatambua kuwa ‘baba’ na ‘mama’ na kusema kuwa haifai kuwa hivo kwani hakuna siku mchungaji wako anaweza kuchukua nafasi ya wazazi wako hata jua litokee magharibi.

“Huu ni ujinga kumuita mchungaji babako au mamako. Mchungaji sio mama yako, mchungaji sio baba yako. Usiniite baba, mimi si babako, mimi ni mchungaji wako,” mchungaji huyo alihubiri.

Alisema kuwa wachungaji wengine wanafanya makusudi kutaka waitwe baba au mama kwa sababu wanajua kuwa neno la mzazi halina ubishi na kuitwa hivo maanake wanataka neno wanalolisema lisiwe na maswali yoyote kutoka kwa waumini.

Mkurugenzi mkuu wa MCSK, Ezekiel Mutua alionekana kukubaliana na kauli hiyo ya Kiamah akisema kuwa wachungaji wengine wanalenga kuwadumaza akili waumini ili kujinufaisha kutokana na kuitwa baba au mama.

Kulingana na Mutua, kumuita mchungaji baba au mama ni kuwakosea heshima wazazi waliokuzaa.

“Kumwita Mchungaji mama au baba kwa kweli ni kuwadhalilisha wazazi halisi na ni njia inayotumiwa na wadanganyifu kupotosha mamlaka ya mzazi. Mchungaji wako si baba au mama yako. Hawawezi na hawapaswi kamwe kuchukua mamlaka na nafasi ya mzazi,” Dkt Mutua alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa ni wakati umefika kwa waumini kama hao kutokomezwa katika jamii kwani wanapotosha vizazi kwa mahubiri kama hayo aliyoyataja kuwa ya kipuuzi.

“Uzushi huu lazima urekebishwe ili kuondoa upuuzi kanisani na kurejesha utulivu katika jamii,” Mutua alikemea.

Je, ni vizuri kwa mtu kumuita mchungaji wake kama baba au mama?