Alikiba apata mpenzi mpya? Picha hizi zazua ukakasi, amtaja mrembo huyu 'kipenzi changu'

Alikiba si mtu wa kuweka hadharani mambo yake ya kifamilia na wengi wamekuwa wakishindwa kujua hatima ya ndoa yake na mkewe wa kwanza Amina Khalef.

Muhtasari

• Mwaka jana kulikuwa na uvumi kwamba Alikiba na mkewe Amina Khalef walitalikiana kutokana na mrembo aliyecheza kama vixen kwenye wimbo wa UTU.

• Hata hivyo, Alikiba hajawahi kulizungumzia hilo wazi na wiki jana alidokeza kwamba huenda hawakutalikiana, akisema yeye bado ameoa.

Alikiba apiga picha na mrembo huyo na kumtaja kama 'kipenzi changu', wengi wahisi penzi limeota.
Alikiba apiga picha na mrembo huyo na kumtaja kama 'kipenzi changu', wengi wahisi penzi limeota.
Image: Instagram

Msanii wa muda mrefu wa Bongo Fleva, Alikiba amepata mpenzi mpya, mwaka mmoja baada ya uvumi kuzuka kwamba wameachana na mke wake Amina Khalef kutoka Mombasa Kenya.

Msanii huyo alipakia msururu wa picha na mrembo Jenifer Jovin maarufu Niffer kwenye Instagram yake wakiwa wamependeza kwenye jezi ambazo zilikuwa na nembo ya ‘Team Kiba’.

Haitoshi, mrembo huyo ambaye ni mtangazaji kwenye Instagram yake alitumia moja ya picha yake akiwa na Alikiba huku wakiwa wametizamana kwa mahaba, kama picha ya utambulisho wake kwenye profaili yake.

Niffer alipakia video ya wawili hao jinsi walivyokuwa wakipiga mapozi mbalimbali kwa ajili ya picha hizo na wengi walihisi kwamba kuna Zaidi ya kile ambacho kilikuwa kinaonekana kwa macho, kwani walikuwa wanataniani kweney video hiyo wakitagusana na kupetiana peti.

Alikiba aliunda jezi hizo za ‘Team Kiba’ kama njia moja ya kuchangia kwenye wakfu wake wa kuwasaidia watoto njiti, na katika kuzitangaza, alimwita Niffer kama ‘kipenzi changu’.

“Jersey blue na off-white zote zipo lengo ni kuchangia usifikirie bei jali quality na mchango wako ️Mimi pamoja na kipenz changu @_.niffer._ @_.niffer._ tunakukumbusha kuwachangia watoto njiti kununua jezi ambayo itakua ni sehem ya kununua vifaa vitakavyowasaida waweze kuishi,” Alikiba aliandika kwenye moja ya machapisho yake.

Hata hivyo, licha ya wengi kudhani kwamba Alikiba na Niffer walikuwa na hisia Zaidi ya uhusiano wa kibiashara, msanii huyo alizidi kusisitiza na kuhimiza kwamba watu wanunue jezi hizo katika duka linalomilikiwa na mrembo huyo kwa bei za rejareja ili kuwachangia watoto waliozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa tumboni – njiti.

Ni wiki moja tu tangu Alikiba alipoweka wazi kwamba yeye ni mume wa mtu na wala hakutalikiwa kama ambavyo wengi wamekuwa wakihisi kwa takribani mwaka mmoja sasa.

Ikumbukwe msanii huyo si mtu wa kuweza kuzungumzia au kuweka mambo yake ya kifamilia hadharani na hivyo imekuwa vigumu kwa wengi wa mashabiki wake kujua ukweli na mustakabali wa ndoa yake na Amina Khalef.