Ezekiel Mutua aahidi kumsaidia Stevo Simple Boy

Ezekiel alisema Stevo ni mwanamuziki mwenye kipaji cha kuigwa na itakuwa jambo la kushtukiza sana kuona taaluma yake ya muziki ikififia.

Muhtasari

• Mutua ameeleza nia yake ya kumsadia mwanamuziki anayedaiwa kukumbwa na matatizo ya kifedha, Stevo Simple Boy.

• “Hatuwezi kupoteza talanta kama hiyo. Mwambie ana kaka na tutamsaidia. Nikiweza kukutana naye nitashukuru," Mutua alisema.

Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki za muziki Kenya, MCSK Ezekiel Mutua
Mkurugenzi mkuu wa chama cha hakimiliki za muziki Kenya, MCSK Ezekiel Mutua
Image: Facebook//EzekielMutua

Afisa mkuu mtendaji wa MCSK  Ezekiel Mutua ameeleza nia yake ya kumsadia mwanamuziki anayedaiwa kukumbwa na matatizo ya kifedha, Stephen Otieno Adera almaarufu Stevo Simple Boy.

Ezekiel akizungumza na wanahabari alisema Stevo ni mwanamuziki mwenye kipaji cha kuigwa na itakuwa jambo la kushtukiza sana kuona taaluma yake ya muziki ikififia.

“Hatuwezi kupoteza talanta kama hiyo. Mwambie ana kaka na tutamsaidia. Nikiweza kukutana naye nitashukuru. Tuna wageni tunaweza kumuunganisha nao ili aweze kushirikiana nao kimuziki. Tutasuluhisha hili, yuko katika mikono salama,” Ezekiel aliwahikishia wanahabari.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Stevo na mke wake Grace Atieno kufichua kuwa mwanamuziki huyo anatatizika kifedha na hata wamewahi kulazimika kulala bila kutia chochote kinywani.

Grace alidai kuwa usimamizi wa Stevo Simple Boy ulikuwa ukimiliki akaunti zake za mitandao ya kijamii, kwa kile alichokitaja kama kunyanyaswa na kampuni hiyo na kuwa na udhibiti kamili wa maisha yake.

 “Tunapitia magumu ni ile tu huwezi kutoka nje kuomba mtu nini na nini, tunavumilia tu. Wakati mwingine tunagombana kutokana na hizo tu changamoto lakini ukimwambia aende aongee na meneja wake mambo ya hela ajisimamie mwenyewe anaogopa,” Grace alisema.

Baada ya Stevo Simple Boy na mke wake kujitokeza na kudai kudhulumiwa na Meneja wake. Kampuni hiyo ilijitokeza na kufutilia mbali mkataba baina yao na msanii huyo.

Kulingana na kampuni hiyo, Men In Business walieleza kughadhabishwa kwao na mwanamuziki huyo kwa kile walichokitaja kuwa kuharibiwa jina na tuhuma zisizo za ukweli.

“Kufuatia tuhuma zisizo sahihi na zisizo halali, na uongo mwingi ambao umetolewa ambao umeharibu sifa ya kampuni, ndiyo maana timu nzima imekaa na kutoa uamuzi kwamba tutoke nje ya mkataba. ,” mwakilishi wa MIB alisema.

Mkataba wa Stevo Simple Boy na Men In Business ulikatizwa rasmi Jumatatu, Juni 26, siku mbili tu baada ya mkewe kudai kuwa msanii huyo anatatizika kifedha na kwamba usimamizi umekuwa ukimnyanyasa.

Kutokana na mkataba wake kufutiliwa mbali mwanamuziki huyo kutoka Kibera alitangaza uamuzi wake wa kujisimamia katika kazi ya sanaa.

“Sai mimi nimeamua kuwa meneja kivyangu nikiwa na mke wangu na rafiki zangu watatu pamoja na wakenya wote kwa jumla. Kama mtu anataka kunisupport wakuje kwangu mimi binafsi.”