Miaka iliyoliwa na nzige imerudishwa - Edday baada ya wanawe kuanza masomo Marekani

Kabla ya kuondoka nchini kwenda Marekani, Edday alifichua kwamba alikuwa amekaa kwenye ndoa na Samidoh kwa kipindi cha miaka 15 ambayo alisema ilionekana kupotea baada ya ujio wa Nyamu.

Muhtasari

• Wiki jana, Edda yalifanikisha kuwaweka wanawe katika mfumo wa masomo Marekani, ishara kwamba hamna dalili yoyote ya kurejea nchini hivi karibuni.

Edday Nderitu.
Edday Nderitu.
Image: Instagram

Mkewe Samidoh, Edday Nderitu ni mama mwenye furaha baada ya kufanikisha ndoto ya wanawe kukubaliwa kuendeleza masomo yao nchini Marekani.

Wiki jana, Radio Jambo ilielewa kwamba Edday Nderitu alifanikiwa kuwaingiza wanawe katika mfumo wa masomo Marekani.

Hii ni baada ya kuondoka humu nchini na watoto wote watatu miezi kadhaa iliyopita katika kile kilitajwa kuwa ni ziara ya likizo ndefu.

Lakini hatua ya kuwaingiza wanawe shuleni Marekani ilizua dhana tofauti, wengi wakielewa kwamba huenda Edday Nderitu hana mpango wa kurudi humu nchini tena, baada ya kuzozana na mumewe kisa Karen Nyamu ambaye pia ana watoto na Samidoh.

Baada ya kufanikisha hilo, Nderitu alikwenda kwenye kurasa za mitandao yake ya kijamii na kuandika ujumbe wa kufarijika akinukuu Biblia kwamba hatimaye miaka yake iliyoliwa na nzige imerejeshwa kwake na Mungu.

“Nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na tunutu, na mharibu, na mkata. Jeshi kubwa lilitumwa kati yenu.Yoeli 2:25,” alinukuu Biblia.

Mwezi Mei, Edday alifichua katika aya ndefu kwamba alikuwa amekaa kwenye ndoa na Samidoh kwa kipindi cha miaka 15 lakini akadokeza kwamba asingependa kuendeleza muda huo iwapo Samidoh ameamua kuoa mwanamke wa pili – Karen Nyamu.

Nderitu alisema kuwa muda wote alikuwa ameweka mawazo yake wazi kabisa kwa Samidoh kwamba yeye hata wakati mmoja asingefanya udhubutu wa kuwalea wanawe katika ndoa ya mitala.

Kwa muktadha huo, aliongeza akisema kwamba sababu yake kuhamia Marekani na wanawe ilikuwa ni ili kumlinda binti yao mkubwa tineja kutokana na msongo wa mawazo kisaikolojia, ili asije akashuhudia jinsi wazazi wake walikuwa wanaparurana kisa ujio wa mwanamke mwingine.