Carrol Sonie azidiwa na hisia kuulizwa iwapo Mulamwah anamsaidia kulea mtoto

Muhtasari

• Sonie alimtaka Kioko kumuuliza Mulamwah swali hilo kwani yeye ndiye yuko katika nafasi nzuri ya kujibu iwapo anasaidia katika malezi au la.

Carrol Sonie.
Carrol Sonie.
Image: Instagram

Muigizaji Carrol Sonie alionekana kuzidiwa na hisia baada ya mwandishi wa habari za mitandaoni Nicholas Kioko kumuuliza swali iwapo baba wa mwanawe – Mulamwah – anamsaidia katika malezi na matunzo ya binti yao Keilah.

Japo hakuweza kujibu moja kwa moja swali hilo, Sonie alionekana kuegemea upande kwamba huenda Mulamwah tangu alipoweka wazi katika mitandao ya kijamii kuwa mtoto huyo si wake, hajawahi rudisha fikira nyuma na pengine huenda hatoi matunzo yoyote kwa ajili ya mwanao.

Sonie alimtaka Kioko kumuuliza Mulamwah swali hilo kwani yeye ndiye yuko katika nafasi nzuri ya kujibu iwapo anasaidia katika malezi au la.

“Aaah, kusema ukweli hizo stori huwa sitaki kuongelea sana unajua tushatoka huko. Cha umuhimu sasa hivi ni kwamba Keilah ako vizuri, anakua. Lakini pia nahisi mtu huyo uliyemtaja [Mulamwah] anafaa kuulizwa swali sahihi, swali kama [Sonie alicheka] … sote tunajua kwamba alimkataa mwanawe. Sijui mbona hammuulizi swali hilo kwamba ni kweli ulikataa mwanao,” Sonie alijibu kwa kujikaza.

Sonie alisisitiza kwamba mambo huenda yakawa sawa kama kweli waandishi wa habari za udaku watamuuliza Mulamwah maswali sahihi kuhusu makuzi ya binti yake Keilah.

“Inafaa mmuulize maswali kama ‘Keilah ni mwanao, ndio ama hapana’” alitoa mwongozo wa maswali kwa waandishi wa habari za mitandaoni.

Hata hivyo, Sonie alidinda kabisa kutoa mwanga kuhusu suala zima la ni nani baba wa mtoto wake, akisema kuwa hilo si jambo la msingi kwa sasa hivi bali yeye anachozingatia ni kuona mwanawe anakua katika siha na mazingira mazuri.

Sonie alikiri kwamba ana udaku mwingi ambao uanahusiana na suala na ni nani baba wa mtoto wake, lakini akaahidi kwamba asingeusema sasa hivi bali siku moja ataweka kila kitu wazi kupitia chaneli yake ya YouTube.