Mwanangu ana miaka 8, nimemnunulia gari la kumpeleka shuleni - Kennedy Rapuda atamba

"Gari hilo lina thamani ya takribani 830,000 na nina dereva kwa ajili yake ambaye ninamlipa kila mwezi,” aliongeza.

Muhtasari

• Rapudo alizidi kusema kwamba yeye upande wake anafaa kutoa karo ya shuleni na kila mwezi kutuma shilingi elfu 30 za malezi.

Kennedy Rapudo.
Kennedy Rapudo.
Image: Screengrab

Kennedy Rapudo, ambaye mara nyingi mpenzi wake Amber Ray anamtambulisha kama tajiri kwa mara nyingine ameonesha utajiri wake kwa kusimulia jinsi anavyompa mwanawe maisha ghali.

Rapudo ambaye ana mtoto na mwanamke mwingine kabla ya kukutana na Amber Ray alisema kwamba licha ya kutengana na mama mtoto wake, bado anahakikisha kwamba mwanawe huyo anapata kumega vizuri kutokana na utajiri wake ambao hajawahi kuweka wazi unatokana na mitikasi ipi.

Akizunumza na Mungai Eve, Rapudo alifichua kwamba mwanawe sasa ana umri wa miaka minane lakini tayari amemnunulia gari la kumpeleka shule na pia kumuajiri dereva maalum kwa ajili yake tu.

“Mtoto wangu siku yake ya kuzaliwa ni Septemba 12, nimemnunulia gari na pia nimeajiri dereva wa kumpeleka shuleni na kumrudisha nyumbani kwa mama yake,” Rapudo alisema kwa tambo nyingi.

“Mimi hulipa karo yote na niliongea na uongozi wa shule wakasema basi lao la wanafunzi haliwezi kwenda mpaka sehemu mtoto wangu anaishi na mamake, kwa hiyo nililazimika kwenda hadi Mombasa ili kumnunulia gari. Gari hilo lina thamani ya takribani 830,000 na nina dereva kwa ajili yake ambaye ninamlipa kila mwezi,” aliongeza.

Mjasiriamali huyo aidha alipata kuzungumzia kisa ambacho kimegonga vichwa vya habari hivi majuzi  baada ya kudai kwamba mama wa mwanawe alikataa Rapudo alionane na mwanawe.

Rapudo alisema kwamba baada ya mama mwanawe kukataa kumuona mwanawe, alikwenda mahakamani na kumshtaki mama mwanawe kwa kukata asionane na mwanawe.

Rapudo alizidi kusema kwamba yeye upande wake anafaa kutoa karo ya shuleni na kila mwezi kutuma shilingi elfu 30 za malezi.

Septemba mosi, Rapudo anadai kwamba alimtumia vocha ya laki na elfu 30 kwa ajili ya ununuzi wa vitu vya nyumbani lakini mama mwanawe alirudisha vocha hiyo akisema kwamba alitaka pesa taslimu.

“Nilimtuma vocha ya 130k lakini alikataa, alirudisha akisema kwamba alitaka taslimu,” Rapudo alisema.

“Elfu 30 inafaa kuwa ya chakula na bidhaa za chooni, mimi nilimtumia vocha kwa sababu niliona ni sawa na pesa taslimu lakini yeye akairudisha sijui alifikiria nini,” aliongeza.