Harmonize azidisha juhudi za kumuingiza Hamisa kwenye himaya ya Konde Village

Kwa muda sasa, Harmonize amelipigania penzi lake na Hamisa mpaka kufikia hatua ya kuchapisha picha na maneno ya ‘BFF’ kwenye tsheti.

Muhtasari

• Safari hii, Harmonize pia amepiga hatua nyingine kwa kuweka picha yake na ya Hamisa wakiwa kama mume na mke.

Harmonize na Hamisa Mobetto
Harmonize na Hamisa Mobetto
Image: Instagram

Licha ya kuwa na ufahamu fika kwamba Hamisa Mobetto ni mpenzi wa mtu kwa sasa, msanii Harmonize amekuwa sikio lisilosikia dawa kwa kuendeleza juhudi na majaribio mara kwa mara kumtongoza mjasiriamali huyo ambaye pia ni mpenzi wa zamani wa Diamond.

Harmonize tangu aanze kunogesha juhudi zake kumfukuzia Hamisa kumuingiza kwenye himaya ya Konde Village, juhudi zake nyingi tu zimekuwa zikigonga mwamba lakini haonekani kukata tamaa hata.

Safari hii, Harmonize pia amepiga hatua nyingine kwa kuweka picha yake na ya Hamisa wakiwa kama mume na mke wake ambayo ilichorwa kwa kuhaririwa na wachoraji hodari.

Mchoraji huyo aliwachora Hamisa kwa mbele na nyuma yake Harmonize akiwa amechomoza kichwa chake kwenye shingo la Hamisa na aliipakia picha hiyo kama ishara iliyomkosha kweli kweli na kuandika “ila walimwengu bana”.

Kwa muda sasa, Harmonize amelipigania penzi lake na Hamisa mpaka kufikia hatua ya kuchapisha picha na maneno ya ‘BFF’ kwenye tsheti lakini pia kwa kipindi kimoja alinukuliwa akisema kwamab yuko tayari hata kuwa mchepuko wake baada ya kutaarifiwa kwamba jamaa Kevin kutoka Togo ndiye anayelimega bato.

Wiki jana akiwa kwenye shoo yake mjini Dar es Salaam, Harmonize alimualika Hamisa lakini ndio hivyo tena hakuweza kutokea, jambo ambalo baadae Harmonize alifunguka kwamba lilimkwaza sana.

Wakati anazidisha mipigo yake kwenye moyo wa Hamisa, mrembo huyo yuko katika kipindi kigumu sana cha maisha yake ambapo watu mitandaoni wamekuwa wakimvuta kuhusiana na mpenzi wake wa zamani Diamond kumsusa mwanawe wakati aliwakusanya wanawe kutoka kwa kina mama tofauti na kwenda nao Rwanda lakini akamkatia umeme mwanawe Dylan.