Stevo ataja kusumbuliwa na vichuna kama sababu ya kuhama Sekula kwenda Gospel

Kwa sasa, Stevo anafanya kazi na meneja Chingiboy Msado na produsa chipukizi Freshi Kid Onthe Beat.

Muhtasari

• Hata hivyo, anapojiandaa kuingia katika miziki ya injili, Stevo alisema kwamba jina halitabadilika bali litasalia.

Stevo atangaza vita dhidi ya Tanzania
Stevo atangaza vita dhidi ya Tanzania
Image: Screengrab

 Baada ya msanii Stevo Simple Boy wiki jana kutangaza kwamba mwezi ujao ataingia rasmi katika kutunga miziki ya injili na kuitupa katika kaburi la sahau miziki ya kidunia, sasa rapa huyo matata amefichua sababu kuu ya kufanya uamuzi huo wa ajabu.

Akizungumza na mwanablogu Trudy Kitui, Stevo Simple Boy alisema kwamba ameamua kumkimbilia Mungu baada ya kubaini kwamba katika ulimwengu wa ngoma za kidunia, wasichana wengi walijitokeza wakitaka kuning’inia kwa jina lake ili kujizolea umaarufu.

Kwa njia moja au nyingine, hilo lilimkwaza na akakaa chini na kutafakari kwamba faraja ya kweli ni katika Mungu.

“Mimi narudi injili, haya mambo watu husema kwamba injili haina hela, tunaenda kuitoa kwa akili zao. Injili kuna hela ukiimba nyimbo za maana. Watu wakae wapole, labda mimi tu ndio ninaweza rudisha injili penye inastahili kuwa. Hapo awali vichuna walikuwa wanataka umaarufu na jina langu, lakini sasa hivi Stevo Simple Boy si yule wa kawaida, ni yule wa injili,” Stevo alisema.

Stevo alitaja japo kwa kugusia tu kwamba tayari ameshatimba studioni na kufanya kolabo na msanii wa kitambo Rojo Mo – wimbo ambao utashuka mapema mwakani, halafu pia ngoma za binafsi.

Stevo aliwamiminia sifa watu wanaomuongoza katika safari yake mpya ya muziki akiwemo Chingiboy, meneja wake lakini pia na produsa chipukizi Fresh Kid on the Beat – ambao wamekuwa wakishirikiana kumweka katika mstari sahihi kisanaa kufuatia kubuma kwa uongozi wa zamani.

Hata hivyo, anapojiandaa kuingia katika miziki ya injili, Stevo alisema kwamba jina halitabadilika bali litasalia lakini akasema kama atapata mtoto basi atabadilisha jina hilo.

“Kama nitapata mwana nitabadilisha lakini si sasa hivi. Kuhusu idadi ya watoto, hapo inategemea na Mungu atakavyonipangia,” alisema.

Msanii huyo hakusita kumpa sifa na koja la maua msanii Bunny Asila ambaye kwa njia ya kipekee wimbo wake aliomshirikisha Christina Shusho kutoka Bongo ndio umekuwa kichocheo kikubwa kumvutia kwa injii.

Itafahamika kwamba hata hapo awali, Stevo licha ya kuimba nyimbo za sekula, maudhui yake yamekuwa muda wote safi na ya kuhimiza matabaka yote katika jamii, lakini pia kwa wakati mmoja alikuwa anajihushisha na vibao vya injili – ila safari hii sasa anaingia mazima kwenye injili.