Spika wa bunge amvisha koja la maua Diamond baada ya kushinda MTV EMA 2023

"Anapopata hii heshima nje ya mipaka yetu, tunapata picha kwamba huyu kijana si kwamba anafanya kazi nzuri nchini, na hata huko kwingine wanamkubali " alisema spika.

Muhtasari

• Diamond alituzwa kama msanii bora wa bara zima la Afrika akiwashinda majina wakubwa kama Asake, Libianca na Burna Boy.

Diamond Platnumz
Diamond Platnumz
Image: Instagram

Spika wa bunge la Jamhuri ya Tanzania, Dkt Ackson Tulia amekuwa mtu maarufu wa hivi punde kumpa pongezi msanii Diamond Platnumz kufuatia ushindi wake kwa tuzo za MTV EMA 2023 jijini Paris Ufaransa wikendi iliyopita.

 Diamond alituzwa kama msanii bora wa bara zima la Afrika akiwashinda majina wakubwa kama Asake, Libianca na Burna Boy.

Akizungumza katika kipindi cha asubuhi kituoni Wasafi FM, spika Tulia alisisitiza kwamba anamheshimu sana Diamond kama mmoja wa vijana ambao wanatoa mwelekeo mwema kwa vijana chipukizi katika tasnia ya Sanaa.

“Kwanza nimpongeze sana, sio kwamba nampongeza leo tu, huwa nampongeza kila siku. Ni kijana ambaye amefanya kazi kubwa sana katika hili eneo la Sanaa ya muziki, lakini pia ule ukubwa wa kazi si kwamba ametufanay sisi leo kukaa hapa lakini ukubwa wa kazi unapimwa kwa wale watu ambao unakuwa wewe umewasaidia kufikia malengo yao,” Spika Tulia alisema.

Kiongozi huyo aliweza kutambua mchango mkubwa ambao Diamond amefanya katika lebo ya Wasafi kwa kuwatoa wasanii wakubwa ambao wanafanya vizuri kimuziki na wengine hata kujisimamia na kufungua lebo zao wenyewe.

“Ametengeneza ajira kwa watu wengi sana. Anapopata hii heshima nje ya mipaka yetu, tunapata picha kwamba huyu kijana si kwamba anafanya kazi nzuri nchini, na hata huko kwingine wanamkubali na wanajua anafanya kazi nzuri. Kwa hiyo ni lazima mtu anayestahili heshima, apewe heshima yake, na huyu anastahili heshima na mimi namheshimu sio kwa sababu tu ni marafiki bali ni kutokana na kazi yake nzuri,” aliongeza.