Wabunge waungana kumchangia hela msanii Professor Jay 'live' bungeni

Mbunge mmoja alitoa hoja ya kila mbunge kuchangisha 50k na mwingine akasema 200k lakini spika alitaka kila mmoja kutoa kadri ya uwezo wake kwa siku mbili; Alhamisi na Ijumaa kabla ya Jay kukabidhiwa.

Muhtasari

• Mbunge mmoja kwa jina Aida Kenani alisimama na kutoa hoja kwa wabunge wote kumchangia.

• Wabunge wengi wlaipiga makofi na hivyo kutoa kiashiria kwa spika kwamba hoja hiyo ilikuwa imeungwa mkono.

Professor Jay akiwa bungeni.
Professor Jay akiwa bungeni.
Image: Screengrab

Adhuhuri ya Alhamisi msanii na aliyekuwa mbunge Professor Jay alikuwa mgeni katika bunge la Jamhuri ya Tanzania kufuatia mwaliko wa spika Dkt Ackson Tulia.

Baada ya kumtambulisha kwa wabunge, spika alisema kwamba msanii huyo ana jambo laki kuelekea mwishoni mwa mwezi huu ambapo atakuwa anazindua rasmi wakfu wake wa kutoa hamasisho kuhusu gonjwa la figo.

Ikumbukwe Jay aliugua kwa Zaidi ya siku 460 hospitalini baada ya kupata tatizo la figo lake kufeli na hivi majuzi katika mahojiano yake ya kwanza, alisema kwamba hicho ndicho kimekuwa kichocheo kikubwa kwa wakfu wake kuzaliwa.

Wabunge wote wakiwa wametambua matatizo ambayo amepitia katika kipindi cha miaka miwli iliyopita, akitumia mwaka mmoja na miezi kadhaa hospitalini, walitoa hoja ya Jay kuchagiwa pesa.

Mbunge mmoja kwa jina Aida Kenani alisimama na kutoa hoja kwa wabunge wote kumchangia akisema kwamba angependelea kama inaruhusiwa kufanyika bungeni, basi kila mbunge atoa angalau shilingi elfu 50.

Mbunge mwingine Joseph Musukuma pia alitoa hoja kama hiyo, lakini yeye atakata kila mbunge atoe angalau shilingi laki mbili, laki moja ikienda kwa wakfu na nyingine ikimsaidia Jay moja kwa moja.

“Professor Jay amekuwa mbunge mwenzetu humu ndani na tumefanya naye kazi amelisaidia taifa na kushiriki majanga mengi ambayo watu wengi walikuja humu ndani bunge tukapitisha azimio la kuchangia.”

“Sasa kwa hali ile na kwa vile umetangaza atakuwa na uzinduzi wa wakfu, ushauri wangu naomba kwak mheshimiwa spika, ningependekeza kulingana na yeye jinsi alivyo mbunge mwenzetu, tumchangie shilingi laki mbili kwa maana hii, moja iende kwa wakfu na nyingine imsaidie yeye,” Musukuma alisema.

Baada ya spika Tulia kubaini kwamba idadi kubwa ya wabunge walipiga makofi kuashiria kukubaliana na hoja hiyo, aliipitisha lakini akataka kusiwekwe kiwango maalum cha kutoa.

“Waheshimiwa wabunge kwa makofi mliyopiga mengi mengi yanaashiria kwamba hoja ya kumchangia mheshimiwa Jay tunaiunga mkono lakini hata hivyo kuna pendekezo limetoka kuhusu kiasi pia. Kwa sababu humu ndani pia kuna utofauti wetu, ningependa kila mmoja atoe kadri ya yeye anavyoweza kwa sababu wengine wanaweza toa Zaidi ya hapo ikamsaidia Zaidi.”

“Kwa hivyo kwa nia ile ile ambayo mmepiga makofi humu ndani, nawaruhusu hawa wasaidizi wapiti huko wakusanye hiyo michango kati ya leo na kesho halafu atakabidhiwa michango mtakayochanga,” spika Tulia alisema.