Diamond ammwagia hela nyingi Zuchu baada ya mrembo huyo kumuimbia kimahaba jukwaani

Aliingia kweney begi na kuanza kuchomoa viburunguti vya noti kadhaa huku akimkabidhi Zuchu moja baada ya kingine.

Muhtasari

• Zuchu alitimba jukwaani na msanii huyo mpya – D Voice wakiimba kwa njonjo kabla ya watu kuwamiminia hela.

• Hata hivyo Diamond naye hakuachwa nyuma, alijongea karibu na jukwaa kama shabiki yeyote aliyekoshwa na uimbaji wa Zuchu.

 

Diamond na Zuchu
Diamond na Zuchu
Image: Screengrab//YouTube

Kwa mara nyingine wasanii wapenzi, Diamond na Zuchu wameendelea kuoneshana mapenzi mubashara kwa kuimbiana kimahaba na kuzawadiana.

Usiku wa Novemba 16, Diamond alikuwa anamzindua msanii mwingine ambaye anakalia kigonda cha kitinda mimba katka lebo ya WCB ambacho kimekuwa kikikaliwa na Zuchu tangu mapema 2020.

Zuchu alitimba jukwaani na msanii huyo mpya – D Voice wakiimba kwa njonjo kabla ya watu kuwamiminia hela.

Hata hivyo Diamond naye hakuachwa nyuma, alijongea karibu na jukwaa kama shabiki yeyote aliyekoshwa na uimbaji wa Zuchu.

Aliingia kweney begi na kuanza kuchomoa viburunguti vya noti kadhaa huku akimkabidhi Zuchu moja baada ya kingine wakati mrembo huyo anaangaza tabasamu kwenye panda lake la uso.

Zuchu alisimama kwa tabasamu la kutoamini mkononi akiwa ameshikilia mabunda ya noti kabla ya Diamond kuomba kipaza sauti na kuanza kuimba kiitikio cha Zuchu kuhusu mahaba yalivyotabahari.

Diamond na Zuchu kwa Zaidi ya mwaka mmoja wamekuwa wakioneshana dalili zote za kuwa kwenye mahusiano, kwa wakati mmoja wakiashiria kwamba walikuwa tayari kwa hausi yao mwaka jana siku ya wapendanao ya Valentino.

Hata hivyo, baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwamba wawili hao hawana uhusiano wowote Zaidi ya ule wa bosi na mfanyikazi wake – na kwamba wanachokiigiza hadharani kama mahusiano ni njia moja ya kuchangamsha genge tu ilimradi miziki iende.