"Kwani movie moja utarudia mara ngapi jamani?" Akothee auliza wanaozungumzia Omosh

Mama huyo wa watoto 5 alisisitiza kwamba stori za Omosh aliziacha mwaka 2023 na kuwataka wote wanaoumia kutokana na kuachana naye kupona mapema na kusonga mbele na maisha.

Akothee
Akothee
Image: Instagram

Siku chache baada ya Akothee kuwajibu mashabiki wake kuhusu ndoa yake iliyovunjika mwaka jana miezi 5 tu baada ya kuifunga na aliyekuwa mpenzi wake Denis Shweizer, maarufu kama Mr Omosh, mjasiriamali huyo amewataka mashabiki wake kusahau kitu chochote kumhusu mtu huyo kutoka Uswizi.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Akothee alisema kwamba baada ya kuzungumzia stori hiyo, amepata wanablogu wengi wakimzungumzia pakubwa katika mitandao ya kijamii wengi wakijikita katika hadithi kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake na Mr Omosh.

Msanii huyo alisema kwamba ni maajabu kuona akizungumziwa na kutagiwa katika mitandao ya kijamii kisa stori za ndoa yake iliyovunjika wakati hakupata kuzungumziwa wakati anahangaika kuanzisha shule yake au kusaidia watoto maskini kujiunga na shule za upili.

Kwa msisitizo, Akothee alisema kwamba mambo na Mr Omosh aliyaacha mwaka 2023 na kuwataka wote wanaozungumzia hayo kupona na kusonga mbele na maisha, huku akisisitiza kwamba ya Omosh ilikuwa tu kama filamu ambayo mtu hutazama mara moja na kuisahau.

“Sijui kwanini wanablogu wananiweka tagi kila mahali, nimefanya nini mwaka huu? Sijawahi kuwaona wakipost Akothee Academy au hata watoto niliowapeleka shuleni sasa hivi wananitag ni ma what? Nadhani nilikuwa nimemaliza masuala ya familia na masuala ya Omosh 2023. Ni mwaka mpya na hewa safi. Hawa watu hawajaheal . Kwani movie Moja utarudia mara ngapi jamani?” Akothee alisema.

Hili linakuja wiki moja baada ya Akothee kufichua kwamba kile kilichotokea baina yake na Omosh mwezi Aprili mwaka jana haikuwa harusi bali ilikuwa ni shoot ya video yake.

Mjasiriamali huyo mama wa watoto wanne alisisitiza kwamba Omosh hakuwa kiwakilishi cha mpenzi wake bali alikuwa kama vixen wa kuongeza nakshi katika hafla hiyo.