• “Nimerudi kutoka kwa vivuli, nguvu zaidi kuliko hapo awali. Mungu Wangu Hujainiangusha 🙏.”
Produsa maarufu wa muziki wa nchini Kenya kati ya mwaka 2018 hadi 2022, Magix Enga amejing’amua mwenyewe baada ya juhudi za kufunga kazi kutoka kwa baadhi ya wahisani wema.
Enga ambaye kwa muda tangu atoweke machoni pa tasnia ya muziki kwa muda wote alikuwa akionekana katika mazingira tata wengi wakihisi anasumbuliwa na msongo wa mawazo alisaidiwa wiki chache zilizopita na wahisani kuhakikisha anajirudi na kuendelea na shughuli zake.
Baada ya juhudi hizo kuzaa matunda mema, Enga hatimaye ameonekana kujitambua tena na amerudi mitandaoni kuwashukuru watu wote ambao hawakuwahi kupoteza matumaini kwake.
Aliwataja baadhi ya watu waliosimama naye kumpitishia mchakato wa kurekebika kitabia na kuachana na matumizi ya vitu ambavyo vilikuwa vinamsababishia unyongovu na kusema kwamba hayuko tayari kuangusha juhudi zao tena.
“Nimerudi kutoka kwa vivuli, nguvu zaidi kuliko hapo awali. Mungu Wangu Hujainiangusha 🙏.”
“Asante kwa wote ambao hawakuwahi kupoteza imani nami, Willy M Tuva, Asila Bunny, Nebert Nebo, Big Afrique Studios, Kerry Lens, DJ Sule, na hasa mke wangu wa ajabu ambaye alisimama upande wangu katika yote. Big up kwa marafiki na mashabiki wangu pia… mmekuwa mkiuliza Enga alienda wapi… Enga amerudi ‼️ Wakati wa kutengeneza muziki mzuri usio na wakati,” produsa huyo mwenye kipaji alisema.
Enga ambaye alikuwa akihangaika katika jiji la Nakuru alifichua pia kwamba amepata makazi mapya katika jiji la Eldoret na kusema kwamba huo utakuwa mwanzo mpya katika mazingira mapya kuendeleza shughuli zake za kuzalisha miziki.
“Ninaporudi kwenye mwangaza, ninabeba usaidizi wa timu ya ajabu na imani thabiti ya Home Town yangu mpya :Eldoret. Pamoja, tutaandika hadithi ya uthabiti, ukombozi, na shukrani,” alisema kwa faraja tele.