Mbunge wa Mumias East Peter Salasya alikuwa miongoni mwa umati mkubwa wa watu waliojitokeza Githunguri nyumbani kwa familia ya Brian Chira kumpa buriani.
Salasya alishangazwa na umati mkubwa wa vijana ambao walijitokeza katika hafla ya safari ya mwisho ya tiktoker huyo aliyefariki wiki mbili zilizopita katika ajali ya barabarani.
Mwanasiasa huyo kijana alisema kwamba Chira alikuwa na ushawishi wa kuvuta umati mkubwa wa vijana, jambo ambalo hakuna mwanasiasa anayeweza kufanya.
“Chira alikuwa mshawizi mkubwa kwa vijana wa kizazi cha sasa, mkiangalia hapa, hakuna mwanasiasa hata mmoja, ambaye anaweza kuvuta umati mkubwa kama alivyofanya yeye katika msiba wake. Wale watu ambao nimeona hapa leo sijaamini macho yangu, na ni kwa sababu ya ule ushawishi ambao ndugu yetu amekuwa nao,” Salasya alisema.
Baada ya kumaliza kutoa rambirambi zake, Salasya alitoa mchango wake wa shilingi elfu 40 kumsaidia nyanya yake Chira.
Mapema asubuhi ya Jumanne, maelfu ya jumuiya ya TikTok nchini walifurika katika barabara za kuelekea Githunguri kwa ajili ya kumzika Chira.
Chira alikuwa tiktoker aliyejizolea umaarufu kutokana na video zake zenye utata ambazo muda mwingi zilimpata akiburuzana mabega na baadhi ya watu kimaadili.