Butita kuandama na rais Ruto katika ziara ya USA kukutana na rais Joe Biden ikuluni White House

Eddie Butita alimshukuru rais Ruto kwa kumchagua kuwa miongoni mwa watu atakaoongozana nao katika ziara hiyo yenye haiba ya aina yake.

Muhtasari

• Ziara hiyo itang’oa nanga Alhamisi ya Mei 23 na rais Joe Biden anatarajiwa kuwa mwenyeji wa rais Ruto na kundi lake kutoka Kenya, katika ikulu ya White House.

Butita
Butita
Image: Instagram

Mchekeshaji aliyegeuka na kuwa mjasiriamali katika uzalishaji wa kidijitali, Eddie Butita amejawa na furaha baada ya rais William Ruto kumtaja miongoni mwa kundi la Wakenya atakaoandamana nao katika ziara rasmi ya mwaliko wa rais wa Marekani, Joe Biden.

Ziara hiyo itang’oa nanga Alhamisi ya Mei 23 na rais Joe Biden anatarajiwa kuwa mwenyeji wa rais Ruto na kundi lake kutoka Kenya, katika ikulu ya White House.

Akionyesha furaha yake, Eddie Butita kupitia ukurasa wake wa Instagram alichapisha picha akiwa amestarehe na kumshukuru rais Ruto kwa kumchagua kuwa miongoni mwa watu atakaoongozana nao katika ziara hiyo yenye haiba ya aina yake.

“Kuondoka kwenda Marekani leo. Asante Mheshimiwa Rais William Samoei Ruto kwa kunichagua kuandamana nawe katika Ziara ya Kiserikali ya Marekani iliyoandaliwa na Rais wa Marekani Mheshimiwa Rais Joe Biden,” Butita alisema.

Awali, iliripotiwa kwamba rais Ruto katika ziara yake ya Marekani, atazuru studio za uzalishaji muziki za Tyler Perry na washikadau wengine kadhaa katika mfumo wa ikolojia wa Hollywood ili kuwashirikisha jinsi wanavyoweza kufanya kazi na wbunifu wa Kenya.

Kwa nadharia hii, Butita ambaye ni mmoja wa wabunifu tajika katika kizazi cha sasa alisema kwamba atawakilisha washikadau wenzake katika tasnia hiyo vilivyo, akisema kuwa ni Dhahiri rais Ruto anajali maslahi ya wakuzaji maudhui.

“Ukweli kwamba mimi ni sehemu ya ujumbe wa Mkuu wa nchi ni ishara tosha na tunafurahi kwamba tasnia ya ubunifu ni sehemu ya mazungumzo ambayo tutakuwa nayo katika safari hii,” Butita alisema.