Bahati afichua kwa nini anaogopa kurudi katika sanaa ya injili baada ya kutimukia sekula

“Vibaraka wako wengi kwenye kanisa kuliko kwenye dunia ya sekula. Wakati mtu unafanikiwa watu wanajumuika pamoja kwa haraka ili kukuangusha katika sekta ya injili kuliko katika sekta ya Gengetone.”

Muhtasari

• Bahati alikiri kuwa yeye si mwokovu sana kuliko wengine mtandaoni lakini akasema jambo moja analolijua ni kuwa watu wote wanahitaji kuomba msamaha na kunyenyekea kwa Mungu.

BAHATI
BAHATI
Image: Facebook

Aliyekuwa msanii wa injili na mshindi wa tuzo za Groove, Kevin Kioko Bahati amefunguka kuhusu kudidimia kwa Sanaa ya injili nchini Kenya katika miaka ya hivi karibuni.

Kupitia msururu wa maelezo kwenye insta story zake, Bahati alisema kwamba Kenya itasalia kuwa ngome kuu ya kutoa wasanii wa injili lakini tunakoelekea huenda ikawa vigumu kwa taifa hili kupata wasanii wakubwa wa injili kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.

Msanii huyo alisema kwamba Mungu amehamisha kibali hicho kwa mataifa kama vile Nigeria na Rwanda kwa kile alitaja kuwa Kenya wainjilisti waliopewa kibali hicho walianza majivuno, chuki wenyewe kwa wenyewe na wengine kuwa vibaraka.

“Kenya ilikuwa na itazidi kuwa sehemu ya uamsho wa injili lakini huenda hatutakuwa katika nafasi ya kutoa chapa kubwa za injili kama ilivyokuwa miaka 10 iliyopita. Kwa nini? Sababu ya Mungu kuhamisha kibali hicho kwenda Nigeria na Rwanda…”

“Sisi kutazamia kwa watu kama Sinach na rafiki yangu Israel Mbonyi si kwamba Kenya hatujui kuimba vizuri, au hatuna nyimbo nzuri za injili, hapana. Ukweli ni kwamba vipaji ambavyo Mungu alikuza kanisani vimegeuka na kuwa na chuki za wenyewe kwa wenyewe,” Bahati alisema.

Msanii huyo alisisitiza kwamba vibaraka wengi wanapatikana kanisani kuliko vile wapo kwenye dunia ya sekula.

“Vibaraka wako wengi kwenye kanisa kuliko kwenye dunia ya sekula. Wakati mtu unafanikiwa watu wanajumuika pamoja kwa haraka ili kukuangusha katika sekta ya injili kuliko katika sekta ya Gengetone.”

“Huwa sipendi kuzungumzia sana kuhusu masuala ya kanisa na najua wanajijua watasema natafuta kiki lakini ukweli ni kwamba mimi huogopa sana kukaribia hii industry juu najua vile wanachukiana,” alisema.

Bahati alikiri kuwa yeye si mwokovu sana kuliko wengine mtandaoni lakini akasema jambo moja analolijua ni kuwa watu wote wanahitaji kuomba msamaha na kunyenyekea kwa Mungu.

“Kitu najua tunahitaji kuomba msamaha na kuacha kuwa vibaraka ili Mungu atupeleke katika kiwango kingine, bila hivyo, mimi naomba Mungu aendelee kuinua Arbantone mkijifanya manaibu wa Yesu na nyinyi ni vibaraka,” alimaliza.