Juhudi za Harmonize kuomba Meek Mill kolabo zafeli rapa wa USA akidai hajawahi msikia

Harmonize ajaribu kujitambulisha kuwa ni msanii maarufu kutoka Afrika Mashariki, lakini Mill alionekana kutokubaliana na hilo akisisitiza kwamba hamjui na wala hajawahi sikia msanii kwa jina ‘Harmonize’.

Harmonize na Meek Mill
Harmonize na Meek Mill

Mashabiki wa Harmonize wamepigwa butwaa baada ya juhudi za msanii huyo kuangukia pua akiomba kufanya kolabo na rapa maarufu wa Marekani, Meek Mill.

Harmonize alichapisha picha ya mazungumzo ya faragha na Meek Mill na kujaribu kujitambulisha kuwa ni msanii maarufu kutoka Afrika Mashariki, lakini Mill alionekana kutokubaliana na hilo akisisitiza kwamba hamjui na wala hajawahi sikia msanii kwa jina ‘Harmonize’.

Katika mazungumzo hayo, Harmonize alionekana akiwa amemuandikia jumbe nyingi Mill akimuomba kolabo lakini Mill alimjibu akimuuliza yeye ni nini.

“Wewe ni nini? Msanii Afrika? Sijawahi kusikia,” Mill alimwambia wazi wazi Harmonize.

Hata hivyo, mkurugenzi huyo wa lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide alimjibu akimwambia kuwa yeye ni msanii  na pia kuwaomba mashabiki wake kufurika katika ukurasa wa Meek Mill ili kumfikishia ujumbe kuhusu ombi la msanii wao kuomba kolabo.

“Mtu Fulani tafadhali ambieni Meek Mill kuhusu ni nani Konde Boy. Kwa kweli nina hamu sana ya kufanya kazi na yeye, mimi ni shabiki wake mkubwa,” Harmonize aliandika.

Harmonize alipigwa na butwaa kutojulikana na Meek Mill licha ya juhudi zake za awali kufanikisha kolabo na wasanii kama Bobby Shmurda na wasanii wanaofanya vizuri kutoka Nigeria Burna Boy na Ruger.