Kate Actress aomba radhi kwa majibu ya ukali kwa waliodai ziara ya USA ilifadhiliwa na serikali

Kate alisema kwamba nafsi yake ilimsuta kutokana na jinsi alivyokuwa akiwajibu baadhi ya watu waliokuwa wakimsisitizia kukubali kuwa ziara yake ya Marekani ilifadhiliwa na serikali kwa pesa za mlipa ushuru.

Muhtasari

• Kate kwa kutamauka na kughirika alijipata akiwajibu vikali kwa kebehi, jambo ambalo saa 24 baadae lilikuja kumkwaza na kumtuma kuomba msamaha kwa  baadhi ya majibu yake.

Kate Actress.
Kate Actress.
Image: Instagram

Muigizaji Kate Actress amejitokeza na kutoa barua ya kujishusha kwa kuomba msamaha kwa baadhi ya watu aliowakwaza katika mtandao wa Instagram kutokana na majibu yake makali kwa hoja zao kuwa safari yake kwenda Marekani ilifadhiliwa na serikali.

Kate alisemekana kuwa miongoni mwa watu Zaidi ya 20 walioandamana na rais Ruto mwezi jana kwenda mwaliko rasmi wa rais wa Marekani, Joe Biden katika ikulu ya White House.

Hata hivyo, siku kadhaa baada ya kurudi, Kate Actress aliwashangaza wengi kujiunga na makundi ya vijana kushinikiza kuangushwa kwa mswada wa fedha 2024, ambao wengi wanahisi haufai taifa katika uchumi wa sasa unaosuasua.

Kutokana na hili, wengi walimuona kama kibaraka na kufurika kwenye ukurasa wake Instagram kumuita majina wakitilia shaka kujitoma kwake kwenye maandamano.

Kate kwa kutamauka na kughirika alijipata akiwajibu vikali kwa kebehi, jambo ambalo saa 24 baadae lilikuja kumkwaza na kumtuma kuomba msamaha kwa  baadhi ya majibu yake.

“Ningependa kutoa msamaha wangu wa dhati kwa baadhi ya matamshi yasiyo sahihi ambayo nilitoa katika ukurasa wangu wa Instagram. Baada ya tathmini ya kina, nimegundua kwamba majibu yangu yalikuwa tu ya kebehi kuhusu madai kwamba ziara yangu kwenda Marekani ilifadhiliwa na serikali, ninasisitiza kwamba haikufadhiliwa,” alisema.

“Hata hivyo, nimegundua kwamba nilipaswa kujibu kwa njia ya heshima Zaidi, ningependa kutumia nafasi yangu katika mitandao ya kijamii kupigania haki za kila mmoja wetu kama wananchi, na nitatumia nafasi yangu kupigania uboreshaji wa taifa letu,” Kate aliongeza.