Eric Omondi akita kambi katika lango la bunge kulalamika kupitishwa kwa mswada wa fedha 2024

Hata hivyo, maafisa wa polisi wa kutuliza ghasia walifika kwa wingi na kumtaka kuondoka eneo hilo wakijaribu kumpiga farasi, jambo ambalo Omondi alipinga vikali akiwataka wampige yeye na si mnyama.

Muhtasari

• Omondi alisema kuwa mswada huo ni dhalimu kwa Wakenya na kumtaka rais Ruto kutoupitisha na kuwa sheria, katika kile alisema kuwa sheria hiyo itawaumiza wengi.

Image: HISANI

Mchekeshaji aliyejiongeza na kuwa mwanaharakati, Eric Omondi amewashangaza wengi kuelekea katika lango la bunge la kitaifa kulalamika kupitishwa kwa mswada tata wa fedha wa mwaka 2024 licha ya kuwa katika kipindi cha kumuomboleza kakake mdogo, Fred Omondi.

Katika video na picha zinazoenezwa kwenye mitandao ya kijamii mchana wa Ijumaa, Omondi alionekana na mavazi ya rangi nyekundu akiwa juu ya farasi katika barabara ya majengo ya bunge.

Omondi alielekea na farasi wake hadi mbele ya lango kuu la kuingia bungeni n kulalamika kwamba lengo ni kuukataa mswada wa fedha ambao ulipitishwa Alhamisi alasiri.

Omondi alisema kuwa mswada huo ni dhalimu kwa Wakenya na kumtaka rais Ruto kutoupitisha na kuwa sheria, katika kile alisema kuwa sheria hiyo itawaumiza wengi.

“Ajenda ni kuukataa mswada wa fedha 2024, kama bunge la Kenya limepitisha mswada huu, hii nchi haitakuwa kawaida tena, huo ndio ujumbe nimetumwa kuwaambia. Rais asithibutu kutia saini mswada huo kuwa sheria, ni mswada dhalimu na inaumiza mama mboga, watu wa kansa, vijana, imegusa nepi na mpaka dawa ya watoto.”

“Sasa tunaambia wabunge wale ambao walipitisha, nimekuja tu kuwaambia, ilikuwa kufikishwa bungeni mara ya pili, wasiupitishe,” aliongeza.

Hata hivyo, maafisa wa polisi wa kutuliza ghasia walifika kwa wingi na kumtaka kuondoka eneo hilo wakijaribu kumpiga farasi, jambo ambalo Omondi alipinga vikali akiwataka wampige yeye na si mnyama.

“Nipigeni mimi, msipige mnyama, nimekuja kufa. Mkipitisha hii nchi haitakuwa sawa. Watu 204 hamwezi amulia watu milioni 54,” alisema kabla ya polisi kumnyanyua kutoka juu ya farasi na kumtupa ndani ya gari la polisi.

Mwanaharakati huyo amejitokeza kushiriki maandamano ambayo yameshuhudia mamia ya vijana wiki hii kujitokeza, kipindi ambacho maandalizi ya mazishi ya kakake, Fred Omondi yanaendelea.

Fred Omondi alifariki Jumamosi iliyopita katika ajali ya barabarani na anatarajiwa kuzikwa Jumamosi ya Juni 29 nyumbani kwao Sega, kaunti ya Siaya.