Eric Omondi atilia mashaka mazingira ambayo kaka yake Fred Omondi alifariki, “Hai’add up”

“Na kama kaka yangu alikuwa amebebwa kwa pikipiki, huyu mtu ako wapi? Tulienda tukaona pikipiki, ni kweli ajali ilikuwa mbaya, tuliona mpaka kulikuwa na damu hapo, lakini eti mwenye pikipiki eti hayuko. Na hiyo impact! Eti yeye alitoka mbio…"

Muhtasari

• Omondi alisema kwamba huenda kuna mkono wa mtu katika kifo cha mdogo wake na kwamba hakuna jinsi ingekuwa ajali ya kawaida kakake kufa huku dereva wa bodaboda akiponyoka mauti.

Eric Omondi na Fred Omondi katika shoo yao ya mwisho pamoja mapema Juni
Eric Omondi na Fred Omondi katika shoo yao ya mwisho pamoja mapema Juni
Image: Facebook//Choma Choma Lounge, Kisii

Mwanaharakati Eric Omondi amejitokeza na kufafanua kwa nini aliamua kujitokeza kuandamana kupinga mswada wa fedha wa 2024 licha ya kuwa katika kipindi cha maombolezo ya kifo cha kaka yake, Fred Omondi.

 Akizungumza wikendi iliyopita wakati alikuwa anajiandaa kusafiri kurudi kijijini kutoka Nairobi, Omondi alionekana kutilia shaka mazingira tata ambayo mdogo wake alipatana na umauti wake.

Omondi alisema kwamba huenda kuna mkono wa mtu katika kifo cha mdogo wake na kwamba hakuna jinsi ingekuwa ajali ya kawaida kakake kufa huku dereva wa bodaboda akiponyoka mauti.

“Baadhi ya watu wamekereka na mimi kwamba ninaomboleza kifo cha kaka yangu, mbona nilijitokeza kuandamana. Kuna dhana, hii ni wiki ya mswada wa fedha, na kila mtu anajua mimi ndiye ninaongoza vita dhidi ya huu mswada. Kwa hiyo inakuwaje kwamba wiki yenye mswada unapitishwa ndio kaka yangu anakufa?” Omondi alihoji.

“Na kama kaka yangu alikuwa amebebwa kwa pikipiki, huyu mtu ako wapi? Tulienda tukaona pikipiki, ni kweli ajali ilikuwa mbaya, tuliona mpaka kulikuwa na damu hapo, lakini eti mwenye pikipiki eti hayuko. Na hiyo impact! Eti yeye alitoka mbio…hiyo ndio maana nilitoka kuandamana kwa sababu nalala naamka naona ama ilikuwa ni ukweli hii dhana nyingine,” aliongeza.

Lakini pia Eric alisisitiza kwamba asingependa sana kujikita katika kudhania kiini cha kifo cha kaka yake, akisema kuwa ukweli wakati mwingien unaweza ukachukua muda, hata Zaidi ya mwaka.

“Hata hivyo, sitaki ku’speculate, kwa sababu nishapoteza kaka yangu. Haya ni maisha, unaweza ukapata ukweli baada ya mwaka. Lakini pia kuhusu hii dhana nyingine, ama walikuwa wanaona watanitoa kwenye reli kupigana dhidi ya huu mswada na tumempoteza Fred, basi haitakuwa kwamba tumempoteza Fred bure. Tulimpoteza kwa nini, ndio maana nilipanda farasi nikaenda bungeni,” alisema.

Kuhusu habari za kifo cha dereva wa pikipiki siku chache baada ya ajali, Eric Omondi alisema kuwa ni uvumi tu anaousikia na wala hajapata mtu wa kumuelekeza kwa familia yake wala kujua makafani ambayo mwili wake umehifadhiwa.

“Sisi tunajua Fred ako Chiromo, yeye [dereva] kama alikufa ako wapi? Juu wengine wanasema alikimbia. Na hiyo ajali ilifanyika karibia alfajiri ya 6am jua limeanza kuchomoza, hakuna mtu hata mmoja angerekodi hiyo video iende tu viral mahali juu ni celeb?” Omondi alizidi kuibua hoja kiasi cha haja.