Robert Burale aeleza kwa nini aliomba Gen Z msamaha kwa niaba ya kanisa

"Mimi pia ni mzazi wa mtoto wa miaka 19, Gen Z. kwa hiyo ninaweza nikawepo kama baba nikawaambia mahali ninaona mnaenda mrama nawarudisha kwenye njia salama," Burale alisema.

Muhtasari

• Burale alieleza sababu yake ya kuomba msamaha akisema kwamba kanisa huwa wanazungumza lakini huwa hawasikilizwi

Mchungaji na mshauri wa kimaisha, Robert Burale Jumapili alikuwa miongoni mwa Wakenya waliojitokeza jijini Nairobi kuwaunga vijana wa Gen Z katika maandamano yao ya Amani kupinga kupitishwa kwa mswada tata wa fedha wa 2024.

Mwishoni mwa juma lililopita, vijana hao walitoa ratiba ya kufurika katika maeneo ya ibada kote nchini ili kueneza ujumbe wao kwa viongozi wa makanisa kutaka wanasiasa wazuiwe kufanya siasa makanisani.

Vijana hao walisema kwamba kwa miaka mingi sasa wanasiasa wamekuwa wakihudhuria ibada katika maeneo ya ibada mbalimbali na baadae kuzua siasa kwenye mimbari, jambo ambalo walionya vikali viongozi wa kidini kwamba hawatakubali hilo.

Vijana hao pia waliilaumu kanisa kwa kukaa kimya wakati wa maandamano ya kupinga mswada huo tata, na sasa Burale amejitokeza kuomba vijana hao msamaha kwa niaba ya dini zima ya Wakristo.

Burale alieleza sababu yake ya kuomba msamaha akisema kwamba kanisa huwa wanazungumza lakini huwa hawasikilizwi, wala si kwamba wamekaa kimya kama ambavo vijana wa Gen Z walikuwa wakiwatuhumu.

“Ndio, ni kweli nilifanya kuomba msamaha kwa Gen Z kwa niaba ya kanisa, si kwa sababu kanisa haizungumzi bali huwa tunazungumza lakini hatusikilizwi. Kwa sababu huwezi ukawaambia Gen Z kwamba ni shauri yenu, hilo litamaanisha hatuko pamoja na wao. Hivyo niliomba msamaha kwa niaba ya kanisa nikiwaambia kama wanahisi kuna mahali tuliwaanusha tunasema samahani,” Burale alisema.

Mchungaji huyo alitetea kanisa akisema kwamba hili limewafungua macho na kwenda mbele watakuwa katika mstari wa mbele kupaza sauti zao kwa mambo ambayo wanaona yanakwenda kombo.

“Na tunatumahi sasa kwenda mbele tutakuwa wenye sauti zaidi na pia tutawamboea, tutaombea serikali na  baada ya kila kitu kufanywa na kuzungumzwa, Mungu sharti asalie kuinuliwa na kuabudiwa.”

Kuhusu iwapo atajiunga kwenye maandamano Jumanne wiki hii kuungana na Gen Z, Burale alisema;

“Sisi kama washauri, wachungaji, ni sharti tuwe karibu na hawa vijana. Mimi pia ni mzazi wa mtoto wa miaka 19, Gen Z. kwa hiyo ninaweza nikawepo kama baba nikawaambia mahali ninaona mnaenda mrama nawarudisha kwenye njia salama. Hatutaki tena kusikia kijana mwingine mdogo amefariki, hatutaki kusikia afisa wa polisi amepoteza maisha, wala biashara yoyote kuharibiwa.”