MP Babu Owino azungumzia video akiruka kwenye ua la bunge waandamanaji walipovamia bunge

Katika video hizo, Babu Owino alionekana akijisatiti kupanda kwenye ua la chuma linalozunguka majengo ya bunge huku vijana wakiwa tayari wamewalemea polisi na kuingia bungeni.

Muhtasari

• Owino pia alituma ujumbe wa rambirambi kwa baadhi ya Wakenya waliopoteza wapendwa wao wakati wa makabiliano hayo ya waandamanaji na polisi katika majengo ya bunge.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kwa mara ya kwanza amezungumzia video na picha zilizomnasa aking’ang’ana kuruka kwenye ua la majengo ya bunge wakati mtafaruku wa maandamano ya vijana wa Gen Z yalipofika bungeni.

Katika video hizo, Babu Owino alionekana akijisatiti kupanda kwenye ua la chuma linalozunguka majengo ya bunge huku vijana wakiwa tayari wamewalemea polisi na kuingia bungeni.

Hata hivyo, mbunge huyo amekanusha dhana zilizoenezwa awali kwamba alikuwa anaruka ua ili kutoroka kutokana na ghadhabu ya waandamanaji, na kusema kwamba alifanya vile ili kujiunga na wananchi kuandamana kupinga mswada wa fedha.

“Niliruka lango la Bunge ili kuungana na Wakenya wenzangu barabarani walipokuwa wakiomboleza kifo cha mmoja wetu aliyeuawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi wakorofi,” Babu Owino alisema.

Owino pia alituma ujumbe wa rambirambi kwa baadhi ya Wakenya waliopoteza wapendwa wao wakati wa makabiliano hayo ya waandamanaji na polisi katika majengo ya bunge.

“Rambirambi zangu kwa familia zote ambazo zimepoteza wapendwa wao bila sababu leo ​​kutokana na mauaji ya kiholela yanayofanywa na Serikali.Vifo vyao havitakuwa vya bure,Tutapambana hadi tushinde,” Owino alisema.

Makabiliano ya polisi na waandamanaji katika majengo ya bunge yaliwaacha kadhaa wakiwa na majeraha ya risasi huku angalau watu 10 wakiarifiwa kufariki wakati wa mtafaruku huo.

Kwa wiki ya pili sasa, vijana wamekuwa wakiandamana kupinga kupitishwa kwa mswada wa fedha 2024 kwa kile wanadai baadhi ya vipengele vyake ni dhalimu.