Bunny Asila kutoa msaada wa kimatibabu kwa mtoto wa miaka 16 aliyepigwa risasi tumboni Githurai

Kwa mujibu wa familia, binti huyo wa kidato cha 3 hakuwa mmoja wa waandamanaji bali alikuwa ameenda kuchukua chakula cha jioni kutoka kwa mamake ambaye ni muuza mboga wakati risasi ya polisi ilimfuma tumboni.

Muhtasari

• “Ningependa kumpa usaidizi na kuwa baraka kwake katika wakati huu mgumu kwake" Asila alisem.

BUNNY ASILA
BUNNY ASILA
Image: FACEBOOK//BUNNY ASILA

Msanii nambari moja wa injili ya Kenya anayeishi nchini Ufini, Bunny Asila amekuwa mtu wa hivi punde kujitokeza na kuonyesha ghadhabu yake kwa matukio ya machafuko yaliyoshuhudiwa wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Asila alipakia msururu wa video za simulizi ya tukio la kutia huruma lililofanyika katika mtaa wa Githurai 45 viungani mwa mji wa Nairobi.

Asila alisikitishwa na jinsi watu wanaodhaniwa kuwa maafisa wa polisi walifyatua risasi kihohola katika mtaa huo duni majira ya jioni ya Jumanne na kuwaua watu kadhaa wakiwemo watoto lakini pia kuwaacha makumi wengine na majeraha mabaya ya risasi.

Simulizi ya mtoto Winfrey Wairimu mwenye umri wa miaka 16 ambaye alijipata katikati ya zogo hilo majira ya saa moja jioni ya Jumanne alipokwenda kumfuata mamake barabarani kuchukua mboga kwa ajili ya kuandaa chajio baada ya kutoka shuleni.

Kwa mujibu wa taarifa, Tabitha Waithera, mamake Winfey Wairimu ni mama mboga katika mtaa wa Githurai, na siku ya mkasa, polisi walikuwa wanafyatua risasi kiholela wakati risasi zilimpata bintiye ambaye alikuwa amefika kibandani kuchukua mboga.

Binti huyo wa kidato cha tatu ambaye alijipata kwenye sokomoko hiyo ya Githurai alipigwa risasi tumboni na kwa sasa yuko katika hospitali kuu ya Kenyatta kwa matibabu.

Tukio hili ambalo liligonga vichwa vya habari siku ya Jumatano lilimgusa sana Bunny Asila ambaye ameonesha nia ya kujitoa kwa hali na mali kusimama na familia hii kwa msaada wa kimatibabu kwa ajili ya mpendwa wao.

Asila ameomba mtu yeyote mwenye anaweza kumuunganisha na familia hii kufanya hivyo ili kunyoosha mkono wake wa kusaidia, kwani kwa jinsi mama yake alivyokuwa anaeleza, ni Dhahiri kwamba ni mtu wa maisha ya chini ambaye ametwikwa mzigo mwingine wa kuhangaikia matibabu ya ghafla kwa bintiye ambaye hakuwa mmoja wa waandamanaji.

“Ningependa kumpa usaidizi na kuwa baraka kwake katika wakati huu mgumu kwake, mtu tafadhali nisaidie kumtafuta ikiwa unamfahamu. Alikuwa ameathirika na matukio ya Githurai,” Bunny Asila alisema.

Awali, Asila alikuwa ameahidi kutoa msaada wa maji na vinywaji kwa waandamanaji katika miji ya Nairobi na Nakuru, ahadi ambayo alitimiza siku ya Jumanne wakati wa maandamano ya kihistoria ambayo yalishuhudia vijana wakiwazidi polisi nguvu na kuingia ndani ya majengo ya bunge kwa kutumia nguvu.