Terence, 2Mbili, Akuku, Dacha miongoni mwa mastaa waliohudhuria ibada ya wafu ya Fred Omondi

Wikendi iliyopita, chama cha wachekeshaji nchini kilikuja pamoja na kufanya tamasha la kumuenzi Fred Omondi kwa mara ya mwisho, katika mgahawa wa Carnivore, na walifanikiwa kuchangisha shilingi milioni 1.1

Wachekeshaji katika ibada ya wafu ya Fred Omondi
Wachekeshaji katika ibada ya wafu ya Fred Omondi
Image: HULIOH//MPASHO

Ibada ya wafu kwa ajili ya marehemu mchekeshaji, Fred Omondi imefanyika asubuhi ya Ijumaa katika makafani ya Chiromo jijini Nairobi.

Katika ibada hiyo, makumi ya wachekeshaji wenza walijitokeza kumpa faraja kaka yake aliyebakim Eric Omondi ambaye pia ni mchekeshaji wa muda mrefu aliyegeukia uanaharakati.

Katika ibada hiyo iliyofanyika katika ukumbi mdogo wa makafani ya Chiromo, wachekeshaji kama vile Sandra Dacha, Terence Creative, 2mbili na wengine walipata nafasi ya kuzungumzia jinsi walivyofanya kazi naye marehemu Fred Omondi.

Wengine pia ambao walijitokeza ili kumpa faraja Eric ni pamoja na MC Jessy, Don Nyachio, Akuku Danger na wengine wengi, kila mmoja akimzungumzia Fred kwa mazuri na ucheshi wake.

Kwa upande wake, Terence alifichua kwamba ni yeye aliyekuwa mtu wa kwanza kabisa kupata taarifa za kifo cha Fred Omondi na kuanza mchakato wa kumtafuta Eric Omondi.

Baadae leo, mwili wa Fred Omondi unatarajiwa kusafirishwa moja kwa moja hadi Sega, kaunti ya Siaya kwa ajili ya maziko hapo kesho Jumamosi.

Omondi alifariki dunia wiki mbili zilizopita jijini Nairobi baada ya pikipiki aliyokuwa ameiabiri majira ya alfajiri kugongana ana kwa ana na matatu.

Wikendi iliyopita, chama cha wachekeshaji nchini kilikuja pamoja na kufanya tamasha la kumuenzi Fred Omondi kwa mara ya mwisho, katika mgahawa wa Carnivore, na walifanikiwa kuchangisha shilingi milioni 1.1