Akothee amwandikia Eric Omondi ujumbe wa kumfariji anapozika mdogo wake Fred Omondi

“Leo naomboleza na wewe ndugu yangu. @ericomondi Juu juu, inaweza kuonekana kudhibitiwa, lakini ndani kabisa, maumivu ni makubwa. Kupoteza mpendwa sio rahisi, na kwa mtu ambaye alikua yatima,"

Muhtasari

• Ibada ya wafu ya Fred Omondi ilifanyika jana Ijumaa katika makafani ya Chiromo ambapo mastaa kadhaa walihudhuria ili kumpa Eric Omondi faraja.

AKOTHEE AMFARIJI ERIC
AKOTHEE AMFARIJI ERIC
Image: HISANI

Msanii na mjasiriamali Esther Akoth maarufu kama Akothee amemuandikia ujumbe wa kumfariji mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi leo hii Jumamosi ya Juni 29 anapomzika mdogo wake Fred Omondi.

Fred Omondi ambaye alifariki baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani wiki mbili zilizopita wakati bodaboda aliyokuwa ameabiri kugongana dafrau na matatu majira ya alfajiri jijini Nairobi anazikwa nyumbani kwao Sega, katika kaunti ya Siaya.

Akothee katika ujumbe wake kwa Eric amemtaka kuwa na moyo wa ujasiri japo kwamba anafahamu ni uchungu mwingi kwa mtu kumpoteza mdogo wake, hata kama kwa nje inaonekana rahisi.

“Leo naomboleza na wewe ndugu yangu.  @ericomondi Juu juu, inaweza kuonekana kudhibitiwa, lakini ndani kabisa, maumivu ni makubwa. Kupoteza mpendwa sio rahisi, na kwa mtu ambaye alikua yatima, ni muhimu zaidi. Hakika ninaelewa undani wa kile unachopitia sasa hivi,” Akothee alimwambia Eric.

Hata hivyo, Akothee alisema Eric atakuwa katika nafasi nzuri kwani mwisho wa siku atakuwa na mtoto na mke ambao atarudi kwao kwa faraja Zaidi baada ya kumpoteza kaka yake wa kipekee aliyekuwa amesalia naye baada ya kaka mwingine kufariki 2018.

“Ndugu, weka kichwa chako juu. Niko pamoja nawe katika safari hii ya upweke ya umaarufu. Baada ya kuhangaika kwa siku nzima, una mke na mtoto wa kurudia. Familia iliyotoka kwako huleta faraja na furaha kubwa. Huo ndio uamuzi bora zaidi uliowahi kufanya. Nakupenda kaka. Poleni sana, na Ndugu yetu na mwenzetu FRED OMONDI apumzike kwa Amani,” Akothee alimaliza.

Ibada ya wafu ya Fred Omondi ilifanyika jana Ijumaa katika makafani ya Chiromo ambapo mastaa kadhaa walihudhuria ili kumpa Eric Omondi faraja.

Baadae, mwili wake ulisafirishwa kwa ndege kutoka Nairobi hadi Kisumu na baade kwa barabara hadi Siaya ambapo atapumziswa.