“Nimekuwa mpinga Ruto tangu nizaliwe 1989!” Vera Sidika ajibu wanaosema hajaandamana

Sidika alisema kwamba kwa wakati mmoja, walibishana na baba yake wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 kuhusu Ruto kuwa rais, akisema familia nzima ilikuwa inampendelea Raila isipokuwa baba yao ambaye alikuwa mfuasi sugu wa Ruto.

Muhtasari

• Sidika alisema msimamo wake ni kama tu wa watu wengine wengi maarufu mitandaoni, kwamba anaupinga mswada huo.

Mwanasosholaiti Vera Sidika amenyoosha msimamo wake kuhusu tuko linaloendelea nchini la Gen Z kuandamana kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024.

Kupitia insta story yake, Vera Sidika ameweka wazi kwamba yeye tangu siku ya kwanza alipozaliwa amekuwa akimpinga rais Ruto na sera zake, akisema kwamba wanaomtuhumu kwa kutomuona akiandamana ni wanafiki.

Sidika alikuwa akisema haya kufuta ukungu uliokuwa umemzingira baada ya kukabiliwa na baadhi ya watumizi wa mitandao ya kijamii ambao walitaka kujua msimamo wake kuhusu mswada wa fedha.

Sidika alisema msimamo wake ni kama tu wa watu wengine wengi maarufu mitandaoni, kwamba anaupinga mswada huo, na kusisitiza kwamba wengine huenda wamenza kumpinga Ruto sasa lakini yeye alianza mwaka 1989 alipozaliwa.

“Nashangaa watu wanasema hawajaniona nikipinga mswada wa fedha, wakati kila siku niko hapa nikichapisha kuupinga mswada huo. Nimekuwa nikipinga tangu 1989 nilipozaliwa, mimi nimekuwa mpinga Ruto tangu siku ya kwanza,” Sidika alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kwamba yeye alikuwa ametabiri hili kutokea mapema kabla hata Ruto hajawa rais.

Sidika alisema kwamba kwa wakati mmoja, walibishana na baba yake wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 kuhusu Ruto kuwa rais, akisema familia nzima ilikuwa inampendelea Raila isipokuwa baba yao ambaye alikuwa mfuasi sugu wa Ruto.

“Nilitabiri hili kutokea, nilibishana na baba yangu wakati wa kupiga kura. Familia nzima likuwa nyuma ya Baba [Raila Odinga] lakini baba alikuwa anaunga mkono Ruto, familia nzima ilikuwa inahisi kama inataka kummeza mazima,” alisema.