Tanasha Donna asitisha kutoa ngoma ili kuwaomboleza waliofariki katika maandamano

Mpaka kufikia sasa, makumi ya vijana wameripotiwa kufariki kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa polisi huku wengine wkiripotiwa kutoweka kwa njia tatanishi.

Muhtasari

• “Single yangu ya kwanza kutoka kwa project yangu ilikuwa itoke leo, lakini tunaomboleza vifo vya mashujaa wetu wachanga, hadi badae,” Donna alisema.

TANASHA DONNA
TANASHA DONNA
Image: INSTA

Msanii Tanasha Donna ametangaza kusitisha kuachia ngoma yake mpya ambayo iliratibiwa kutoka Ijumaa kisa machafuko yanayoendelea humu nchini kufuatia makabiliano kati ya polisi na waandamanaji wanaopinga mswada wa fedha 2024.

Kupitia insta story yake, Tanasha Donna aliwataarifu mashabiki wake kwamba alikuwa ameweka kila kitu tayari kuachilia ngoma yake mpya Ijumaa lakini imembidi kusitisha shughuli hiyo ili kutoa nafasi ya kuwaomboleza waliofariki katika maandamano.

Aidha, mama huyo wa mtoto mmoja ambaye pia ni mpenzi wa zamani wa msanii Diamond Platnumz alisema hana uhakika ni lini tena wimbo huo utatoka, akiwaacha mashabiki wake kwenye mataa.

“Single yangu ya kwanza kutoka kwa project yangu ilikuwa itoke leo, lakini tunaomboleza vifo vya mashujaa wetu wachanga, hadi badae,” Donna alisema.

Machafuko yamekuwa yakishuhudiwa humu nchini, haswa jijini Nairobi na vunga vyake kwa wiki mbili sasa baada ya vijana wa Gen Z kusema ‘punda amechoka’ na kujitokeza kwa wingi kuandamana kushinikiza kutupiliwa mbali kwa mswada huo tata.

Katika maandamano hayo, licha ya vijana hao kutokuwa na silaha yoyote, matumizi ya nguvu kupita kiasi kutoka kwa polisi yameshuhudiwa, kupelekea vifo vya vijana ambao hatia yao ni kuandamana na kudai haki yao.

Hata hivyo, Ijumaa mahakama kuu iliamuru kwamba polisi hawafai kutumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waandamanaji, ikiwemo matumizi ya vitoza machozi, maji ya kuwasha au hata risasi.