Mtangazaji Joyce Gituro aapishwa kama afisa wa mawasiliano ya umma wa kaunti ya Machakos

Gituro sasa atakuwa anasimamia kitengo cha mawasiliano ya umma na ya kidijitali katika kaunti hiyo.

Muhtasari

• Gituro sasa atakuwa anasimamia kitengo cha mawasiliano ya umma na ya kidijitali katika kaunti hiyo.

• Wengine pia walioapishwa ni pamoja na Francis Munyambu na Dkt Juliana Ndunge.

JOYCE GITURO.
JOYCE GITURO.
Image: X//Wavinya Ndeti

Mtangazaji wa muda mrefu kwenye redio, Joyce Gituro ni mwenye furaha baada ya kupata kazi kama afisa wa mawasiliano ya umma katika kaunti ya Machakos.

Gituro alichapisha video kutoka kwa hafla ya kuapishwa iliyofanyika mapema asubuhi ya Jumatatu ya Julai 1 ambayo iliongozwa na gavana Wavinya Ndeti.

Gituro sasa atakuwa anasimamia kitengo cha mawasiliano ya umma na ya kidijitali katika kaunti hiyo.

Wengine pia walioapishwa ni pamoja na Francis Munyambu na Dkt Juliana Ndunge.

“Leo nimeshuhudia kuapishwa kwa Maafisa Wakuu 3 kufuatia kukaguliwa na kuidhinishwa na Bunge la Kaunti ya Machakos. Maafisa hao ni: Francis Munyambu - Idara ya Ukaguzi na huduma za dharura, Joyce Gituro - Idara ya Mawasiliano ya Umma na E-serikali, Dr.Juliana Ndunge - Idara ya Majitaka, Usafi wa Mazingira na Udhibiti wa taka,” Gavana Wavinya Ndeti alisema.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Joyce Gituro alishukuru kwa kuteuliwa kama afisa wa kaunti na kuchukua nafasi hiyo kumshukuru kila mmoja ambaye amekuwa nyuma yake kwa muda mrefu.

“Ninayo mengi ya kusema kuhusu uteuzi huu lakini kwa sasa niruhusu nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake ambazo ni mpya kila kukicha, @governorwavinyandeti kwa kuniamini mimi, binti yangu kipenzi na wanangu wawili wa kiume kwa kunipenda siku zote, mara moja na kwa majaliwa yangu. Wanafamilia kwa kuwa pale na kwa marafiki zangu WOTE kwa kuwa wavumilivu sana kwangu. Hakika acha Bwana aongoze njia kwenye eneo langu jipya. Baraka🙏 ##mamajakes #machakoscounty,” Gituro alisema.