Ng’ang’a amsuta Mbunge Mohamed Ali kuhusu mswada tata wa Fedha

“Jicho Pevu sasa jiangalie mwenyewe Ile jicho pevu ulikuwa nayo ilienda wapi sasa. Mbona huwezi kueleza hii kiinaendelea."

Muhtasari

•Mchungaji alikumbuka maisha ya zamani ya Mohamed Ali kama mwandishi wa habari, ambapo alijulikana kwa uchunguzi na msimamo mkali juu ya haki za binadamu na utawala bora.

•Matamshi yake yanakuja huku kukiwa na hasira ya umma dhidi ya wabunge waliounga mkono Mswada tata wa Fedha wa 2024.

Nganga
Image: HISANI

Mhubiri James Maina Ng’ang’a wa Neno Evangelism Centre amemsuta mbunge wa Nyali Mohamed Ali, almaarufu Jicho Pevu.

Mhubiri huyo mwenye utata alimtaka ajieleze kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2024, ambao Wakenya wengi wameupinga.

Katika video moja kwenye mahubiri yake, Mchungaji Ng’ang’a alimkosoa vikali mbunge huyo, akimlaumu vikali kwa kubadilisha mienendo yake baada ya kuingia kwa siasa.

Mchungaji alikumbuka maisha ya zamani ya Mohamed Ali kama mwandishi wa habari, ambapo alijulikana kwa vipande vyake vya uchunguzi na msimamo mkali juu ya haki za binadamu na utawala bora.

Wakati wa taaluma yake ya uandishi wa habari, Ali alipata jina Jicho Pevu kutoka sehemu yake ya ripoti za uchunguzi na Kuwa mtu anayependwa sana na Wakenya.

“Jicho Pevu sasa jiangalie mwenyewe Ile jicho pevu ulikuwa nayo ilienda wapi sasa. Mbona huwezi kueleza hii kiinaendelea.

Wewe Jicho Pevu ona jicho pevu hii utuelezae nyinyi mmenunuliwa mmepewa pesa ngapi.”

“Hata nimeona watu wako wanasema ulivote yes na wewe ni jich pevu.

Jicho pevu sasa jiangalie mwenyewe tumbo lako. Waongo hao!” Mchungaji Ng’ang’a alifoka.

Kasisi Ng’ang’a aliwaambia watu wajaribu kumkabili, akidai kwamba walinzi wao wangewageuka.

“Ukinijaribu, utajiua. Mlinzi wako atakupiga risasi,” Ng’ang’a aliongeza.

Matamshi yake yanakuja huku kukiwa na hasira ya umma dhidi ya wabunge waliounga mkono Mswada tata wa Fedha wa 2024, ambao wengi wanaona kuwa haujali masaibu ya Wakenya.

Licha ya maandamano makubwa, wabunge wengi walipitisha mswada huo katika hatua zote.

Ni baada tu ya Wakenya kadhaa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa ndipo Rais, ambaye hapo awali aliunga mkono mswada huo, aliamua kuukataa kuutia saini.

Zaidi ya hayo, Rais alisema kuwa uamuzi wake ulitokana na upinzani mkali kutoka kwa Wakenya dhidi ya mapendekezo ya kodi.